Mastaa wa Stars wamkuna Amunike

Muktasari:

  • Amunike aliingoza kwa mara ya kwanza Taifa Stars kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) Cameroon mwakani dhidi ya Uganda.

KOCHA wa Timu ya Taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’, Mnigeria Emmanuel Amunike amekoshwa na viwango vya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Amunike aliingoza kwa mara ya kwanza Taifa Stars kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) Cameroon mwakani dhidi ya Uganda.

Mchezo huo, umalizika kwa suluhu ambayo imeifanya Taifa Stars kukusanyia jumla ya pointi mbili huku ikiwa imecheza michezo miwili kwenye Kundi L.

“Tulipanga kushinda lakini mambo hayakwenda vizuri kutokana na kushindwa kwetu kutumia nafasi chache ambazo tulizitengeneza. Wenzetu walikuwa nyumbani kwa hiyo ilitubidi kucheza kwa kujilinda ili tusipoteze pointi,” alisema Amunike.

Nyota huyo wa zamani wa FC Barcelona ya Hispania amedai kumekiona alichokitegemea kutoka kwa wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania katika mchezo dhidi ya Uganda. Wachezaji hao ni Hassan Kessy wa Nkana ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka na Himid Mao wa Petrojet ya Misri. Wengine ni Thomas Ulimwengu wa Al Hilal ya Sudan, Shaaban Idd Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania, Saimon Msuva wa Difaa El Jadida ya Morocco na Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.