Mastaa hawa wanapiga doo ndefu kwa saa tu, Sanchez, Kane noma

Muktasari:

  • Hilo unaweza kuliona kuwa gumu kwa upande wako, lakini hutarajii kusikia lolote kutoka kwa mastaa wanaocheza safu ya ushambuliaji kwenye Ligi Kuu England kutokana na pesa za maana wanazolipwa.

MAISHA yanataka nini tena zaidi ya kuwa na pesa na kuishi unavyotaka.

Hilo unaweza kuliona kuwa gumu kwa upande wako, lakini hutarajii kusikia lolote kutoka kwa mastaa wanaocheza safu ya ushambuliaji kwenye Ligi Kuu England kutokana na pesa za maana wanazolipwa.

Hii hapa orodha ya washambuliaji mastaa wanaoingiza pesa ndefu kila saa wanayoishi huko kwenye Ligi Kuu England, huku wote wakitokea kwenye ile Big Six katika ligi hiyo.

Alexandre Lacazette - Pauni 833 kila saa

Fowadi huyo wa Arsenal ameanza kumwonyesha kocha wake mpya Unai Emery kile anachoweza kukivuna kama atakuwa anamwaanzisha katika mechi zao.

Lakini kwa Lacazette hana shida, hata kama hachezi, yeye kila saa inayopita basi kwenye akaunti yake ya benki imeingia Pauni 833 kumfanya kwa wiki avune Pauni 140,000.

Alvaro Morata - Pauni 833 kila saa

Mhispaniola huyo huduma yake anaitoa huko Chelsea. Bado hajaonyesha makali ya kumfariji kocha wake mpya Maurizio Sarri, lakini hilo halina uhusiano katika masuala ya mshahara anaolipwa.

Kwa kila dakika 60 zinazopita, Morata akaunti yake inasoma Pauni 833 na kumfanya aweke kibindoni Pauni 140,000 kwa wiki.

Roberto Firmino - Pauni 1,071 kila saa

Jurgen Klopp anajivunia kuwa na huduma ya Mbrazili, Roberto Firmino kwenye kikosi chake. Anafunga mabao muhimu na jambo hilo linamfanya avune kiasi cha kutosha kutoka kwa wababe wa Anfield Liverpool.

Firmino analipwa Pauni 180,000 kwa wiki, ikiwa na maana Pauni 1,071 zinaingia kwenye akaunti yake ya benki kila saa.

Pierre-Emerick Aubameyang - Pauni 1,071 kila saa

Supastaa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang ni mmoja kati ya wachezaji wenye pesa za kutosha kutokana na mkwanja anaopokea kila saa kwa huduma yake anayotoa huko Emirates. Staa huyo wa kimataifa wa Gabon analipwa Pauni 1,071 kwa sasa na hivyo kwa wiki anakuwa anaweka kibindoni Pauni 180,000.

Raheem Sterling - Pauni 1,071 kila saa

Mwingereza, Raheem Sterling mambo yake ni mazuri huko Manchester City.

Kocha Pep Guardiola anampa nafasi ndani ya uwanja na mabosi wake wanamlipa vizuri mshahara wake wa kila wiki.

Kwa wiki, Sterling anapokea Pauni 180,000, hivyo kumfanya avune Pauni 1,071 kwa kila saa anayoishi huko Etihad.

Eden Hazard - Pauni 1,190 kila saa

Supastaa wa Kibelgiji, Eden Hazard aliwatingisha Chelsea kwenye dirisha lililopita la usajili kabla ya kuamua kubaki Stamford Bridge.

Hazard hakuwa na sababu ya kuondoka kwa sababu anapangwa kucheza na mshahara wake ni matata. Staa huyo analipwa Pauni 200,000 kwa wiki, ikiwa ni sawa na Pauni 1,190 kila saa.

Mohamed Salah - Pauni 1,190 kila saa

Kipenzi cha mashabiki wa Liverpool kwa sasa ni Mohamed Salah. Huduma yake anayotoa kwa wababe hao wa Anfield ni matata kabisa na ndio maana hata mshahara wake pia umekuwa mzuri.

Mo Salah analipwa Pauni 1,190 kila saa anayoishu huko Anfield hivyo kumfanya awe anakusanya Pauni 200,000 kwa wiki.

Romelu Lukaku - Pauni 1,190 kila saa

Straika mwili nyumba wa Manchester United, Romelu Lukaku yupo kwenye orodha hii ya washambuliaji wanaolipwa pesa ndefu kila saa wanayoishi. Staa huyo analipwa Pauni 200,000 kwa wiki, hivyo kwa kila saa anayoishi klabu hiyo ya Old Trafford inamlipa Pauni 1,190. Si pesa ya kitoto ukichenji kuwa ya huku.

Harry Kane - Pauni 1,190 kila saa

Tottenham Hotspur kwa sasa inatamba kwelikweli kutokana na kuwa na huduma ya mshambuliaji Harry Kane kwenye kikosi chake.

Hivi karibuni ilimsainisha mkataba mpya wa miaka sita na kumpa mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki, ikiwa ni sawa na Pauni 1,190 kila saa anayoishi na kutoa huduma kwa wakati hao wanaonolewa na Mauricio Pochettino.

Sergio Aguero - Pauni 1,488 kila saa

Kuna wakati Pep Guardiola alitaka kujichanganya kumbania straika, Sergio Aguero na kumpa nafasi Gabriel Jesus, hapo ingekula kwake.

Aguero ni bonge la mshambuliaji na hilo halina mjadala kwenye Ligi Kuu England. Huduma yake huko Manchester City inalipiwa Pauni 250,000 kwa wiki, ikiwa ni sawa na Pauni 1,488 kila saa anayoishi tu, iwe amecheza hadi hakucheza.

Alexis Sanchez - Pauni 2,083 kila saa

Supastaa wa Chile, Alexis Sanchez ndiye mshambuliaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko yeyote.

Staa huyo kwa huduma yake anayotoa Manchester United inamfanya awe analipwa Pauni 350,000 kila wiki.

Ni pesa ndefu, ambayo ukiigawanya utapata kiasi cha staa huyo wa Old Trafford analipwa Pauni 2,083 kwa kila saa anayoishi bila ya kujali amecheza au hakucheza ilimradi tu bado ni mchezaji wa Man United.