Mastaa Yanga waitaja kambi ya Simba ya Uturuki

NYOTA wa Yanga, wanajiamini kinoma kwani wamedai hakuna tofauti yoyote ya kuweka kambi Morogoro na ile ya wenzao wa Simba kule Uturuki na kusisitiza kama kuna mtu anabisha wasubiri Ligi Kuu ianze waone mambo.

Mastaa hao wa Yanga wanaamini huenda wao wakawa na maandalizi mazuri na kutikisa Ligi Kuu kuliko wenzao, hata kama mitaani mashabiki wamekuwa wakiwakejeli kuwa wameishiwa kukimbilia Mji kasoro bahari.

Winga Deus Kaseke aliweka wazi maandalizi ndio yale yale iwe umeyaweka ndani ama nje ya nchi, ila majibu ya ufanisi huja ligi itakapoanza na kuendelea katika msimu ujao unaoanza wiki ijayo.

"Unajua ipo hivi kama akili na mwili wa mchezaji haujawa tayari kupokea mazoezi hilo ndilo tatizo, lakini kwa habari ya kambi kwamba huyo ameenda huku na mwingine kule hiyo sio ishu.

"Binafsi ninajiona tumeandaliwa kikamilifu na Kocha Mwinyi Zahera, tupo tayari kwa ajili ya kumalizia ratiba ya michuano ya Shirikisho Afrika Jumapili dhidi ya USM Alger, kisha tutaendelea na harakati za Ligi Kuu," alisema Kaseke.

Naye beki Abdallah Shaibu 'Ninja', alisema ameona vitu vya msingi katika soka ni nidhamu, umakini na kujituma na kudai tayari wameishapewa mbinu na kocha Zahera, hivyo Ligi Kuu ianze tu wawafunge mdomo wanaoiponda Yanga.

"Yaani hata ukipelekwa Ulaya usipokua na nidhamu ya soka ni kazi bure, nawaomba mashabiki wetu wajiandae kikamilifu kuhakikisha wanatuunga mkono mpaka pale tutakapotimiza malengo yetu," alisema Ninja aliyerithi jezi ya nahodha wao wa zamani, Nadir Haroub Cannavaro ambaye kwa sasa ni meneja wa timu.

Upande wa Emmanuel Martin, alisisitiza wanahitaji kushinda mechi dhidi ya USM Alger ili kuwaaminisha mashabiki wao kwamba wana kikosi imara kisha mengine yafuate.

"Naamini kwa wachezaji tunaounda timu hiyo, tuna uwezo wa kufanya vitu vya kuwastajabisha wengi, ikiwa tofauti na fikra zao, kuweka kambi Morogoro si ishu naona ni sehemu nzuri tu kama nyingine, kikubwa ni maamuzi pale mtu anaona panamfaa," alisema winga huyo aliyetua Yanga akitokea JKU Zanzibar.