Mastaa Yanga SC mtegoni

Muktasari:

  • Emmanuel Martin aliyebakiza mkataba wa miezi sita ndani ya kikosi hicho, alithibitisha kocha aliacha programu kwa meneja wa timu Hafidh Saleh, ili kuhakikisha kila mchezaji anafuata kila kitu kilichopo.

NYOTA wa Yanga wapo mtegoni baada ya Kocha Mkuu wao, Zahera Mwinyi aliyekuwa mapumzikoni kuwaachia programu ya mazoezi na kama watashindwa kwenda naye sawa mara atakapotua leo basi lazima waipate freshi.

Emmanuel Martin aliyebakiza mkataba wa miezi sita ndani ya kikosi hicho, alithibitisha kocha aliacha programu kwa meneja wa timu Hafidh Saleh, ili kuhakikisha kila mchezaji anafuata kila kitu kilichopo.

“Programu aliyoiacha kocha inatufanya tusikae kizembe kwani amesisitiza tukirejea mapumziko aone matunda yake, hivyo inanilazimu kujitunza na kuzingatia mazoezi ya kunifanya nisije nikaongezeka uzito.

“Japokuwa namaliza mkataba wangu Desemba, hainizuii kuendelea kuzingatia programu hiyo inayolinda heshima ya kazi yangu,” alisema Martin.

Naye beki Pato Ngonyani alielezea programu aliyoiacha Kocha Zahera ni kama mtego kwao kwani wasipojiweka fiti wanaweza kuwa matatani ndio maana wamekuwa wakijifua ili kuhakikisha miili yao inakuwa tayari kwa kazi.

Yohana Mkomola chipukizi wa kikosi hicho alitoa mtazamo wake juu ya programu hiyo, inampa ari ya kujituma na kuona atakaporejea awe na hatua nyingine ya kiwango.

“Ukifikiria nilichoagizwa na kocha kinanipa moyo kufanya kwa bidii, pengine kuliko ingekuwa nafanya yale ambayo yapo ndani ya utaratibu wangu, najua atakuwa ametoa akiwa na lengo lake analotaka kuliona akirejea,” alisema.