Mastaa Waliopiga Bao 30 Msimu Mmoja England

Muktasari:

  • Winga huyo wa kimataifa wa Misri yupo kwenye kiwango bora kabisa cha soka lake kwa msimu huu na kumpa raha Kocha Jurgen Klopp huko kwenye kikosi cha Liverpool na wanapambana kumaliza ligi

LONDON ENGLAND


SUPASTAA wa Liverpool, Mohamed Salah amekuwa mchezaji wa nane kufikisha mabao 30 kwa msimu mmoja Ligi Kuu England baada ya kutikisa nyavu kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Bournemouth Jumamosi iliyopita.

Winga huyo wa kimataifa wa Misri yupo kwenye kiwango bora kabisa cha soka lake kwa msimu huu na kumpa raha Kocha Jurgen Klopp huko kwenye kikosi cha Liverpool na wanapambana kumaliza ligi ndani ya Top Four ili kujihakikishia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

kwa sasa rekodi ya kufunga mabao mengi kwa msimu mmoja Ligi Kuu England ni mabao 34 na kwa sababu Liverpool bado wana mechi nne za kucheza, Mo Salah anaweza kuvunja rekodi hiyo kama ataendelea na moto wake wa kupasia nyavu.

Salah kwa sasa amefunga mabao 30. Mastaa wengine waliofikisha mabao 30 ndani ya msimu mmoja Ligi Kuu England ni hawa hapa.

Luis Suarez

Mabao 31

Msimu: 2013/14

Katika msimu huo, Suarez akiwa kwenye kikosi cha Liverpool hakucheza mechi tano za mwanzo kwa sababu alikuwa akitumikia adhabu, lakini baada ya kucheza tu, alifikisha mabao 15 baada ya mechi 10 tu alizokuwa ndani ya uwanja.

Staa huyo wa Uruguay, alionyesha kiwango bora kweli kweli na kumaliza msimu huo akiwa amefunga mabao 31, huku katika maisha yake hayo, hakuwa na hata moja allilofunga kwa penalti, kwa sababu jukumu la mikwaju hiyo ilikuwa kazi ya Steven Gerrard. Kwa sasa Suarez anakipiga huko kwenye kikosi cha Barcelona, ambako amebeba mataji kibao tangu alipohama mwaka 2014 baada ya fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil.

Robin van Persie

Mabao 30

Msimu: 2011/12

Akiwa kwenye kikosi cha Arsenal, straika Robin van Persie katika msimu wake wa mwisho Emirates alishinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu baada ya kufunga mabao 30 kwenye Ligi Kuu England. Baada ya msimu huo kumalizika, supastaa huyo wa Kidachi alitimkia Manchester United baada ya kunaswa kwa Pauni 24 milioni katika usajili wa dirisha la majira ya joto la mwaka 2012.

Alipokwenda Man United alikwenda kutetea Kiatu chake hicho cha dhahabu, huku akifanikiwa pia kubeba taji lake la kwanza Ligi Kuu England ikiwa ni msimu wake wa kwanza tu Man United, lakini ulikuwa msimu wake wa mwisho Kocha Sir Alex Ferguson huko Old Trafford. Van Persie aliwapa Man United taji la 20 kwenye ligi.

Cristiano Ronaldo

Mabao 31

Msimu: 2007/08

Cristiano Ronaldo huyu huyu unamfahamu wewe anayekipiga huko Real Madrid kwa sasa. Kabla ya kutua Santiago Bernabeu kwa mkwanja mrefu wa Pauni 80 milioni, Mreno huyo alikipiga kwenye kikosi cha Manchester United. Katika msimu wa 2007/08, Ronaldo aliingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ya Ligi Kuu England baada ya kufunga mabao 31 ndani ya msimu mmoja.

Ronaldo tangu alipotua Madrid ameboresha zaidi kiwango chake cha kufunga mabao na hivyo kuvunja rekodi kibao kwa kipindi chote alichokuwa na miamba hao wa Ulaya na kubeba nao mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwamo mawili mfululizo, huku kikosi chake kikiwa kwenye hatua ya nusu fainali ya msimu huu wakikabiliwa na mtihani wa Bayern Munich.

Thierry Henry

Mabao 30

Msimu: 2003/04

Arsenal imewahi kuwa na washambuliaji wengi sana waliopita na waliopo kwenye kikosi hicho hadi sasa, lakini haijapata kutokea kama Mfaransa Thierry Henry. Staa huyo aliwafanya mashabiki wa Arsenal kutembea vifua mbele, kwa sababu kuna baadhi ya mechi aliamua mwenyewe kwa uwezo wake na kuifanya Arsenal kutamba kweli kweli kwenye zama hizo.

Katika msimu wa 2003/04, Henry alikuwa kwenye ubora mkubwa sana akifunga mabao 30 kwenye Ligi Kuu England ndani ya msimu mmoja na kumfanya kocha Arsene Wenger afurahie msimu wake baada ya timu hiyo kucheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mechi hata moja kwenye Ligi Kuu England.

Baadaye, Henry aliondoka kwenye Barcelona na kisha New York Red Bulls kabla ya kurudi kwa mkopo Arsenal na sasa ni kocha msaidizi kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ubelgiji.

Kevin Phillips

Mabao 30

Msimu: 1999/2000

Sunderland ambayo haipo kwenye Ligi Kuu England msimu huu, msimu wa 1999/2000 kwenye kikosi chake ilibahatika kuwa na huduma ya mshambuliaji mmoja matata sana, Kevin Phillips.

Staa huyo aliibukia na kutisha kwa mabao kwenye Ligi Kuu England tayari akiwa na umri mkubwa ambapo alifunga mabao 30 katika msimu huu baada ya kuunda kombinesheni matata kabisa ya ushambuliaji sambamba na Niall Quinn kwenye kikosi hicho cha Black Cats.

Tofauti na wachezaji wengine waliofunga mabao 30 kwenye ligi kwamba walikuwa wanacheza timu kubwa zinazojielewa, Phillips yeye alikuwa kwenye timu ya kawaida tu, lakini ubora wake uliifanya timu hiyo kufuzu kucheza michuano ya Ulaya kutokana na mabao ya fowadi huyo veterani.

Alan Shearer

Mabao 34

Msimu: 1994/95

Akiwa kwenye kikosi cha Blackburn Rovers kilichowahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, Alan Shearer alikuwa matata sana na kwa misimu mitatu tofauti alivuka mabao 30 ndani ya msimu mmoja kwenye michuano hiyo.

Kwanza Shearer alifunga mabao 31 katika msimu wa 1993/94, kisha akapiga mabao 34 katika msimu wa 1994/95 na kupiga tena bao 31 katika msimu wa 1995/96.

Kasi yake ya kufunga ndiyo maana inamfanya staa huyo kuwa ndiye kinara wa mabao wa kihistoria katika michuano hiyo ya Ligi Kuu England, huku huduma yake bora kabisa akiwa ameitoa huko Ewood Park.

Shearer alikuwa matata kwa mipira ya kutenga kama penalti na friikiki na alipiga bao tatu tatu kwenye mechi moja mara nyingi tu katika Ligi Kuu England kutokana na kuwa na hat-trick 11 katika ligi hiyo.

Andy Cole

Mabao 34

Msimu: 1993/94

Andy Cole alikuwa matata zaidi wakati alipokuwa Newcastle United kabla hata hajaenda Manchester United ambako alikwenda kuunda kombinesheni matata kabisa ya ushambuliaji na mwenzake Dwight Yorke.

Wakati yupo Newcastle, Cole aliweka rekodi ya kufunga mabao 34 ndani ya msimu mmoja kwenye Ligi Kuu England kwenye msimu wa 1993/94.

Kitu kinachovutia kuhusu mabao hayo ya Cole ni kwamba hakuna hata moja alilofunga kwa penalti. Aliunda kombinesheni matata na Peter Beardsley na kuwa bora kabisa huko St James’ Park kama aliyokwenda kuunda na Dwight Yorke huko Old Trafford.