Mastaa 12 kukatwa Simba, Yanga

Muktasari:

Lakini, habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba, kuna mastaa wa nguvu 12 ambao wamekalia kuti kavu na huenda wasivae jezi za klabu hizo msimu ujao.

KIPINDI cha mabosi wa Yanga na Simba kuonyeshana ubabe ndio kimewadia na tayari joto la usajili limeanza kupanda ndani ya klabu hizo mahasimu.

Lakini, habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba, kuna mastaa wa nguvu 12 ambao wamekalia kuti kavu na huenda wasivae jezi za klabu hizo msimu ujao.

Kwa sasa Simba na Yanga zinakimbizana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini tayari mabenchi ya ufundi ya timu hizo yameanza kukosa imani na baadhi ya nyota wake kutokana na kuwa na viwango duni hivyo, kushindwa kusaidia timu zao mpaka sasa.

Hali tete zaidi ipo ndani ya Simba ambapo, mastaa sita wamepigwa panga akiwemo shujaa wao wa mchezo dhidi ya Lipuli, Laudit Mavugo ambaye ndiye aliifungia timu hiyo bao pekee la kusawazisha.

Mavugo alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Vital’O ya Burundi mwaka juzi, lakini amekuwa na kiwango duni klabuni hapo akifunga mabao 11 tu ya Ligi Kuu mpaka sasa.

Kiwango duni cha staa huyo kimeifanya Simba kuwategemea zaidi Emmanuel Okwi na John Bocco ambao, msimu huu kwa pamoja wamefunga mabao 33.

Staa mwingine ambaye amekutana na panga la kocha Mfaransa, Pierre Lechantre ni kiungo mshambuliaji, Mohammed Ibrahim ambaye ameshindwa kupata nafasi ya kucheza chini ya kocha huyo. Ibrahim alikuwa mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Simba mwaka jana, lakini ghafla upepo umebadilika na sasa anasubiri benchi.

Nyota wengine ambao viwango vyao havijamvutia Lechantre ni beki Jamal Mwambeleko, kipa Emmanuel Mseja, kiungo Mwinyi Kazimoto pamoja na straika, Juma Liuzio.

YANGA MOTO

Huko Yanga nako unaambiwa hakujatulia kwani, kuna mastaa ambao wako mlango wa kuondokea pale Jangwani na kilichobaki sasa ni kukamilisha taratibu za kuachana nao.

Mastaa waliokalia kuti kavu Yanga ni Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Geofrey Mwashuiya, Juma Mahadhi, Matheo Anthony na Beno Kakolanya.

Ngoma, ambaye kabla ya msimu kuanza alisaini mkataba mpya wa miaka miwili alicheza mechi za mwanzo, lakini tangu alipoumia goti mwanzoni mwa Septemba mwaka jana, hajaweza kurejea tena uwanjani.

Kama Yanga wataamua kumuacha Ngoma watalazimika kuvunja mkataba wake ambao, utakuwa umebaki mwaka mmoja jambo ambalo linawapasua vichwa mabosi wa Yanga.

Tambwe, ambaye ameifungia Yanga mabao 45 Ligi Kuu Bara tangu alipojiunga na timu hiyo Desemba 2014, naye anasumbuliwa na goti kama ilivyokuwa kwa Ngoma mechi yake ya mwisho kucheza ilikuwa ya Kombe la FA dhidi ya Reha na alifunga bao moja mwishoni mwa Desemba.

Mahadhi, ambaye alisajiliwa akitokea Coastal Union ameshindwa kuwa na namba ya uhakika katika kikosi cha Yanga na kushindwa kucheza mara kwa mara, lakini mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.

Kwa upande wake, Mwashuiya ambaye alisajiliwa kutoka Kimondo FC ya Ligi Daraja la Kwanza, miaka mitatu iliyopita ameshindwa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza jambo ambalo linamfanya kufunguliwa mlango wa kutokea.

Kakolanya, Matheo na Mwashuiya mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu na kwa jinsi walivyoonesha viwango vyao ndani ya Yanga huenda wakawa miongoni mwa wachezaji ambao wataondoka.

VIONGOZI WAFUNGUKA

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully alisema akili yao kwa sasa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na baada ya hapo ndipo watajua nani anabaki na nani anaondoka.

“Hatujafahamu wachezaji gani ambao tunawaacha au kuwasajili kwani, wote tupo nao ndio maana wengine mikataba yao inamalizika lakini hatujasema lolote, tunataka kumaliza hili la ubingwa kwanza kisha mengine yatafuata,” alisema Tully.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Yanga Hussen Nyika alisema wameshaanza harakati za usajili, lakini mbivu na mbichi zaidi zitafahamika hapo baadaye.