Maskani ya Mwakinyo stori Ulaya tu!

Muktasari:

  • Egginton katika mji wa Birmingham nchini England Jamaa ambao wamekuwa na kufanya mazoezi na Mwakinyo wamesema, ushindi wake umewapa nguvu mpya na sasa wanafanya mazoezi ya kufa mtu ili wafuate nyayo.

Tanga. Kocha pamoja na wachezaji wa Klabu ya Domojiwe ya jijini Tanga wameeleza kufurahishwa na ushindi alioupata Hassan Mwakinyo aliyempa kipigo cha kuokolewa na mwamuzi (TKO) Sam  
Egginton katika mji wa Birmingham nchini England Jamaa ambao wamekuwa na kufanya mazoezi na Mwakinyo wamesema, ushindi wake umewapa nguvu mpya na sasa wanafanya mazoezi ya kufa mtu ili wafuate nyayo.
Wakiwa mazoezini katika gym ya Klabu ya Domojiwe iliyopo nyumbani kwa mama mzazi wa Hassan Mwakinyo mtaa wa Kombezi kata ya Makorora Jijini Tanga, ilikuwa ni kazi tu.
Hassan Nyangasa (23) amesema ushindi wa Hassan Mwakinyo umempa moyo na kwamba, yeye ana uhakika atafika mbali kwa sababu amekuwa akifuata nyayo zake.
Adinan Kassim (18) amesema, atakaporejea Mwakinyo kutoka England atahakikisha anafuatana naye kwenye kila mazoezi ili kupata mafanikio.
Kwa upande wa Hamis Mwakinyo ambaye ni kocha na kaka yake Hassan Mwakinyo amesema, siri kubwa ya mafanikio ya mdogo wake huyo ni nidhamu ya mazoezi pamoja na kutodharau mapambano.
“Mimi binafsi sikushangaa niliposikia, Hassan kashinda kwa sababu najua uwezo wake na siri kubwa ni nidhamu ya mazoezi na kujituma, mbali ya kufanyia mazoezi kwenye gym kila siku asubuhi na jioni huwa anakimbia, kupanda ngazi  za uwanja wa Mkwakwani akirudia mara nyingi,”alisema Hamis.
Hamis ambaye ni mchezaji mstaafu wa Kik box akiwa amecheza katika nchi mbalimbali na kuchukua mikanda kadhaa alisema kuhusu hatma ya Hassan anasubiri atakaporejea nchini ndipo watajua nini kifanyike.
Naye Shaaban Miraji ambaye ni masimamizi wa mazoezi katika jim hiyo alisema tayari mabondia wenzake wa jijini hapa wamejipanga kwenda jijini Dar es salaam kumpokea.