Simba yamchoka Kapombe

Muktasari:

  • Ugonjwa Pulmonary Embolism unaweza kusababishwa na kitu chochote mfano kuumia kwa aina yoyote au kugongana na mtu uwanjani.

Dar es Salaam. Tangu alipogundulika kuugua ugonjwa wa donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu (Pulmonary Embolism) ilikuwa ni ishara kwa beki Shomari Kapombe hatocheza kwa muda mrefu soka la ushindani.

Tangu wakati huo Kapombe ameshindwa kucheza kwa kiwango chake na muda mwingi amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara.

Kapombe alijiunga na Simba msimu huu akitokea Azam, lakini tangu wakati huo ameshindwa kuichezea timu hiyo baada ya kuumia alipokuwa akichezea Taifa Stars dhidi ya Rwanda kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mechi ya kusaka kufuzu kwa fainali za Chan 2018.

Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba alisema “Kapombe yupo kwenye matibabu ya awali ya saa 72, kutokana na hali yake ya sasa hatoweza kushiriki mazoezi na wenzake. Tukifika Dar tutamkabidhi kwa mwenyekiti wetu wa tiba ili aweze kupata uchunguzi zaidi MOI Muhimbili.”

Kutokana na kukaa nje kwa muda mrefu jambo lililofanya uongozi wa Simba chini ya mwenyekiti wa kamati ya usajili,  Zacharia Hans Poppe ni kama imemuweka njia panda Kapombe amepona ila hataki kucheza.

Hans Poppe aliiambia redio Efm jana kuwa, Kapombe amepona ila ni muoga hivyo wamechoka kumvumilia na hawawezi kuendelea kumpa mshahara wa bure.

"Kapombe amepona ila uoga wake mwenyewe, achague  kama anataka kubaki ama akae pembeni hadi atakapokuwa tayari kutumika, uamuzi upo mikononi mwake ,"alisema.

Hata hivyo kauli hiyo ya Hans Poppe ilimshangaza mmoja wa viongozi wa Simba akidai kuwa Simba inajua ilimsajili Kapombe akiwa majeruhi.

"Ninachojua mimi Kapombe bado anaumwa na lengo la kumsajili ilikuwa ni kwa ajili ya mashindano ya kimataifa, sasa inapotokea anaambiwa hivyo ni kama kumuongezea machungu na kumuondoa kabisa kwenye mstari."

"Nadhani hadi kufikia Januari anaweza kuwa na mwelekeo mzuri, ila bado anasumbuliwa labda daktari aseme vipimo vyake vinasemaje,"alisema

Alipotafutwa daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe hakuweza kupokea simu ili kuthibitisha kama Kapombe kapona au la.