Mashahidi 10 kupanda na Manji

MASHAHIDI wasiozidi 10 wa upande wa mashtaka wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili mwanachama wa Yanga, Yusuf Manji, ambaye jana Alhamisi alikana shtaka linalomkabili.

Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis aliyasema kuhusu mashahidi hao kutoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati akimsomea maelezo ya awali (PH).

Akisomewa maelezo hayo ya awali, Manji alikubali maelezo yake binafsi na kukana shtaka linalomkabili. Kwa mujibu wa maelezo hayo ya awali, Vitalis alidai Februari, 2017 walijihusisha na dawa za kulevya na kutumia.

Alidai, siku hivyo aliripoti polisi na kwamba baada ya kuripoti alipelekwa nyumbani kwake Sea View Kivukoni kupekuliwa.

Aliendelea kudai, pia alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo alipimwa haja ndogo (mkojo) na kugundulika una chembechembe za dawa za kulevya aina ya Benzodiazepine na alifunguliwa kesi ya kutumia dawa za kulevya.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Manji alikubali maelezo yake binafsi ikiwamo majina yake na kuwa yeye ni mfanyabiashara na kukana shtaka.

Wakili Vitalis alidai wanatarajia Kuwaita mashahidi wasiozidi 10 kutoa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka. Kesi kuunguruma Agosti 22, 23 na 25, 2017.

Manji alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16, 2017 ambapo anadaiwa kuwa ,  kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin.

Baada ya kusomewa shtaka hilo Manji alikana kuwa  siyo kweli ‘No amekosea’ na kwenye kesi hiyo anawakilishwa na Mawakili Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Mosses Kimaro, yupo nje kwa dhamana baada  mdhamini mmoja kusaini bondi ya Sh 10mil.