#WC2018: Mashabiki wajitenga baharini kukwepa presha fainali Ufaransa vs Croatia

Muktasari:

  • Presha ya fainali hiyo sio kwa mashabiki waliopo Russia pekee, joto la fainali limepanda kwa mashabiki wanaofuatilia fainali hiyo ya kishistoria wakiwa kwenye nchi zao.

Jumapili ndio itakuwa safari ya mwisho iliyoanzishwa pale Moscow, nchini Russia Juni 14, baada ya miamba wa soka Croatia na Ufaransa kuthibitisha ubora na kutinga hatua ya fainali kwenye Kombe la Dunia.
Presha ya fainali hiyo sio kwa mashabiki waliopo Russia pekee, joto la fainali limepanda kwa mashabiki wanaofuatilia fainali hiyo ya kishistoria wakiwa kwenye nchi zao.
Wafaransa wamekuja na kali ya mwaka baada ya mfanyabiashara mmoja kutengeneza baa ndani ya meli iliyoogeshwa kando mwa bahari ili  kuwapa fursa watu wanaotaka kuwa mbali na habari za soka hasa Kombe la Dunia.
Baa hiyo iliyojengwa jijini Paris, Ufaransa, imekuwa kivutio kikubwa wa wateja wasiotaka kuumiza akili zao  kuhusu habari za Kombe la Dunia.
Eneo hilo limekuwa likitoa huduma ya baa na burudani ya muziki tu.
Mmiliki wa baa hiyo inayofahamika Marcpunet, Arnaud Seite alisema nia yake sio kupinga soka bali ni kuwafanya watu wasiopenda presha za timu zao kufungwa waendelee kuburudka na muziki pamoja na huduma za vinywaji zinazotolewa hapo.
Alisema anaungwa mkono na watu wengi wanaofurahia huduma inayotolewa kwenye baa hiyo. Aliongeza kuwa awali walipanga kutokuwepo runinga yoyote kwenye baa hiyo , bali kuwepo na bidhaa tu pamoja na burudani ya muziki. Lakini kwa sasa zimewekwa runinga kwenye baa hiyo.
Mteja Marie alisema kwamba kwa kipindi hiki anapenda kuwa mbali na homa ya Kombe la Dunia ndiyo hasa kimemfanya kupenda kupata huduma kwenye baa hiyo kwa muda wote kwan watu wanakuwa furaha.
Naye Eve alisema anapendelea kushinda eneo hilo kwa sababu ni tulivu na linawafanya kujitenga na habari za ulimwengu wa soka huku wakipumzika na kutulia zaidi.