Mashabiki wagomea mabadiliko ya Guardiola

Muktasari:

  • Wakati huo Martinez alikuwa akipasha, Bayern hadi hapo ilikuwa tayari nyuma kwa mabao ya jumla 4-0 (aggragate) lakini walijivunia uwezo wao na kujaribu kushambulia mara kwa mara.
  • Robben aliongoza mashambulizi vizuri akitoa msaada kuanzia katikati na kuisaidia timu yake kupata kona nne katika dakika saba tu lakini kona hizo hazikuweza kuwapa bao.

KATIKA toleo lililopita kwenye Kitabu cha Pep Confidential, Mwandishi Marti Perarnau aliendelea kuichambua mechi ya marudiano ya Bayern na Real Madrid, safari hii akionyesha namna mabao yalivyokuwa yakiingia huku Bayern ikihaha kujibu mapigo. Sasa endelea…

Wakati huo Martinez alikuwa akipasha, Bayern hadi hapo ilikuwa tayari nyuma kwa mabao ya jumla 4-0 (aggragate) lakini walijivunia uwezo wao na kujaribu kushambulia mara kwa mara.

Robben aliongoza mashambulizi vizuri akitoa msaada kuanzia katikati na kuisaidia timu yake kupata kona nne katika dakika saba tu lakini kona hizo hazikuweza kuwapa bao.

Katika mechi ya kwanza ugenini Bayern ilipata kona 15 na saba kati ya hizo zilikwenda vizuri eneo la goli, lakini katika mechi ya marudiano ya nyumbani walipata kona tisa na ni moja tu waliyoipelaka vizuri eneo la goli.

Pep alitumia muda wa mapumziko kufanya mabadiliko, Martinez akaingia kuchukua nafasi ya Mandzukic na timu ikahamia katika mfumo wa 4-3-3 huku Shweinsteiger akiongoza mbele ya Kroos na Martinez, hii ilifanya kazi vizuri na ikawa msaada, hata hivyo tayari alikuwa amechelewa.

Kuanzia hapo Bayern wakawa wanacheza vizuri, wanaanza na mpira nyuma huku wakitawala mchezo na timu yao ikawa yenye kujipanga vizuri, hali hiyo iliibua ushawishi wa kuhisi kuwapo tofauti kama Javi Martinez angekuwa fiti kiasi cha kutosha kwa mechi ya nyumbani na ile ya ugenini au kama Thiago angeweza kucheza lakini yote kwa yote Bayern ni lazima wakubaliane na ukweli kwamba wameikosa fainali ya ligi ya mabingwa.

Kwa upande mwingine mashabiki wa Bayern nao walianza kupiga kelele kuashiria kutoridhishwa kwao na mabadiliko yaliyofanya kwa kumtoa Ribery na kumuingiza Gotze licha ya kwamba Ribery alikuwa na wakati mgumu kiuchezaji.

Katika wiki zilizofuata Pep alibaini malipo ya kazi aliyoifanya katika mechi hiyo, lakini pia kulikuwa na baya zaidi lililofuata, uwanja mzima ni kama uliguswa na uamuzi wa Pep kumtoa Muller na nafasi yake kuchukuliwa na Pizarro, mashabiki walipiga kelele kukataa mabadiliko hayo, hawakuridhishwa na kile alichokifanya Pep.

Baadaye Pep akakubali kuhusika katika makosa yote kwa majanga yaliyojitokeza, hakumzungumzia mchezaji yeyote kuwa mfano wa kilichotokea badala yake aliwatetea na kuhakikisha hawahusishwi kwa namna yoyote ile katika mjadala wa baada ya mechi.

Aliwaondoa katika shutuma ambazo zingefuata kutokana na kile kilichotokea uwanjani na majanga yote waliyokumbana nayo.

Timu ya Pep ilikutana na kikosi kizuri, Modric na Alonso kwa jumla wao walitawala mielekeo yote ya mpira ilivyokuwa katika mechi hiyo.

Benzema kwa upande wake naye alionyesha umakini katika kuivizia mipira wakati Bale na Ronaldo walicheza vizuri katika kufungua uwanja, waliinasa mipira na kukimbia nayo lango la Bayern.

Badala ya kuweka nguvu na mkazo eneo la kati ili kuwa bora katika eneo hilo, kwa kuwa na viungo wengi na washambuliaji wachache, Bayern waliweka mkazo mbele na hilo likaifanya iwe dhaifu katika udhibiti wa kwenye maeneo.

Katika kipindi chote cha msimu, Pep amekuwa akizungumzia muingiliano kati ya aina yake ya uchezaji na uchezaji wa Kijerumani, baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Dortmund, Pep alisema, “kama tukijazana eneo la penalti na kupiga mashuti ya uhakika, tutapata mabao lakini hatutotawala mchezo.”

Hata hivyo, kwa wakati huo kauli hiyo haikuonekana kuwa na chembe ya ukweli, wamefikisha mipira katika eneo la penalti la kipa wa Real Iker Casillas mara 74 katika dakika zote 180 yaani mechi ya ugenini na nyumbani, na juhudi zao kwenye goli zilikuwa za kawaida mno.

Itaendelea Jumamosi ijayo…