Mashabiki Simba ni mwaka wa kicheko tu

Dar es Salaam. MASHABIKI wa Simba wajiandae tu kwa sasa, kwani Kaimu Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try again' amesema msimu huo wanachama, mashabiki na wapenzi wa Msimbazi hawatakaukiwa na tabasamu kwa mambo mazuri yajayo.
Kiongozi huyo alisema wachezaji wao wanaonyesha kiwango cha juu, wakiwa wamekaa wiki mbili tu na kocha wao mpya Mbelgiji Patrick Aussems, jambo alilodai wanaamini mbele wataona vitu vikubwa vya kiufundi.
"Umefika wakati wa mashabiki wa Simba kusahau machungu yote, yaliyowahi kutokea kipindi cha nyuma, kwani tuna timu nzuri, kikosi kipana, mfano mzuri kocha amekaa na timu wiki mbili tu, lakini wachezaji wanaonekana wanafanya vitu vikubwa uwanjani.
"Kitu kimoja tu mashabiki wanatakiwa kuelewa kwamba, kutoka sare na Asante Kotoko ni kwa vile timu imetoka kwenye maandalizi ya msimu mpya, pia wapinzani wetu nao ni wazuri na wana hadhi kwa uwezo mkubwa walionao."
Try Again aliwataka mashabiki wa Simba kuacha tabia ya kumshinikiza kocha kumpanga mchezaji wanayemtaka, akidai hawajui nini kipo nyuma ya pazia ama mipango ya kocha ni ipi.
"Kwa Simba hii inahitaji mabadiliko makubwa, kwanza mchezaji asipopangwa wajue wazi kocha ana sababu zake, inawezekana ikawa majeraha, kuumwa kwa ghafla, ama nidhamu mbovu, hizo ni kati ya sababu ambazo kocha anaamua kumuweka mchezaji benchi.
"Kila kocha anahitaji mafanikio ndani ya klabu, hivyo haiingi akilini kumuacha mchezaji nje kwa makusudi ambaye anajua  atamsaidia kupata matokeo, tubadilike na tufanye vitu vya kimataifa,"alisema.
Alizungumzia Simba Day kwamba ilikuwa na mabadiliko makubwa kutokana na walivyoifanya kwa mpangilio mzuri, mwitiko wa mashabiki, kuleta timu bora pamoja na wasanii ambao walitumbuiza kwamba walifanya kazi nzuri.