Mashabiki Njombe Mji nusura wamnyonge Banyai timu kupoteza mechi

Muktasari:

Banyai amesema mashabiki wa timu hiyo hawapaswi kumuona yeye kama mchawi aliyesababisha ipoteze mechi tatu za kwanza bali uongozi ulishindwa kutimiza majukumu yao.

Dar es Salaam. Aliyekuwa kocha wa Njombe Mji leo ametangaza sababu za kujiuzulu kufundisha timu hiyo huku akiutaja uongozi kama chanzo cha klabu hiyo kufanya vibaya huku nao mashabiki wakimtishia maisha baada ya mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City.
Banyai amesema mashabiki wa timu hiyo hawapaswi kumuona yeye kama mchawi aliyesababisha ipoteze mechi tatu za kwanza bali uongozi ulishindwa kutimiza majukumu yao.
"Kuna mambo sita ambayo niliyaweka kwenye ripoti ya kiufundi ambayo ni usajili, vifaa vya mazoezi, mechi za kirafiki, kambi, uwanja wa mazoezi na usafiri.
Katika hivyo vitano, kilichotekelezwa ni kimoja tu lakini vingine hapana, sasa katika hali kama hiyo nawezaje kuhukumiwa?
Baada ya mechi ya Mbeya City, nilitishiwa maisha na mashabiki jambo lililomfanya mwenyekiti wa Njombe Mji anishauri kujiuzulu jambo ambalo hata mimi mwenyewe nililiafiki kwa ajili ya usalama wangu," alisema Banyai.
Banyai alisema ameachana na Njombe Mji kwa amani na amelipwa stahiki zake zote.