Mashabiki Mbeya City wapagawa kwa kipigo

Muktasari:

Timu hiyo tangu ilipopanda Ligi Kuu misimu mitatu iliyopita haina rekodi ya kuifunga Yanga Dar es Salaam

Mbeya. Kipigo cha mabao 5-0 walichopata Mbeya City kutoka kwa Yanga  kimewachanganya mashabiki na wadau wa klabu hiyo jijini Mbeya.

Tangu City ipande daraja kushiriki Ligi Kuu Bara haijawahi kupokea kichapo kama hicho zaidi ya rekodi hiyo kuvunjwa na mabingwa watetezi.

Katika mchezo huo mabao ya Yanga yalifungwa na Obrey Chirwa alifunga mabao matatu na Emmanuel Martin alifunga mabao mawili kwenye Uwanja wa Uhuru.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mashabiki wa timu hiyo walisema kipigo hicho kimewasikitisha na hawakutarajia kutokana na timu yao kuwa na kikosi bora.

Mmoja wa mashabiki hao, Wilson Edward kutoka Tunduma alisema "inauma kwa timu yetu kupokea kipigo hicho, ni jambo ambalo hatujazoea tangu timu ianze kushiriki ligi,'.

Alisema pamoja Kocha Mkuu Ramadhan Nswanzurwimo ameomba msamaha, lakini inabidi ajitathimini ili makosa yaliyofanywa yasijirudie.

Naye Japhet Jackson wa tawi la Uyole alisema timu kupoteza mechi tatu mfululizo ni jambo linalowaumiza na kukatisha tamaa ya 'kuisapoti' timu.

"Mabao yote ukiangalia ni uzembe wa mabeki ukianzia na Mkandawile walikuwa wanamtegemea mwamuzi badala ya kucheza mpira, hivyo hivyo kwa golikipa alishindwa kuwasiliana na mabeki wake," alisema Jackson.

Aliongeza "Hadi golikipa Owen Chaima amalize adhabu yake na kurudi uwanjani, City itakuwa teja wa timu nyingi kutokana na huyu anayedaka sasa kutojiamini,' alisema Jackson.