Masau afunika ziara ya Ruvu Shooting Mtwara

Mtwara. Afisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amekuwa kivutio mkoani Mtwara baada ya kuwasili na timu hiyo kwa ajili ya ziara ya siku tatu.

Ruvu Shooting wanatarajia kuzindua tawi lao jipya mkoani humu katika wilaya ya Newala wamewasili  katika tarafa ya Kitangale.

Mara baada ya kuwasili Kitangale, msafara wa Ruvu Shooting ukiwa na Masau ulisimama na kuwasubiri wenyeji wao ambao walikuja kuwapokea na gari ndogo iliyobeba spika kubwa zilizokuwa zinatema burudani mbalimbali za muziki.

Wakazi wa Kitanagele waliusogea msafara wa Ruvu Shooting na kuanza kuhoji yuko wapi Masau Bwire, ofisa huyo alionekana kutabasamu na kuishia kuwatazama.

Masau hakutaka kujitambulisha kwao muda huo na badala yake akajisemea baadaye  "Aiseeh!! Ruvu Shooting inakuwa kwa kasi. Inapendeza."

Safari ya kikosi cha Ruvu Shooting itaendelea baada ya kupokelewa na wenyeji wao kuelekea Makonga ambayo ipo mbele ya Kitangale kwenye wilaya ya Newala.