Martinez, Thierry Henry wanukia Leicester City

London, England. Uongozi wa klabu ya Leicester City, unafikiria kulifumua benchi lake la ufundi na kuingiza sura mpya huku Kocha wa timu ya Taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez na msaidizi wake Thierry Henry wakitajwa kumrithi Claude Puel.

Leicester City ambayo msimu uliopita ilimtimua kocha aliyeipa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu England, Claudio Ranieri kutokana na timu hiyo kufanya vibaya, imeanza kupoteza imani na Claude Puel licha ya kuinasua kwenye janga la kushuka daraja, lakini inaonekana ameshindwa kufikia mafanikio yaliyokusudiwa.

Mmoja wa maofisa wa timu hiyo amefichua kuwa klabu hiyo inatafuta mtu anayeweza kumshawishi Roberto Martinez akubali kutua England kuinoa Leicester ambayo haijapata mafanikio yaliyotarajiwa chini ya Kocha Puel. “Katika mazungumzo yanayoendelea ndani ya uongozi ni kuwa kama Martinez atakataa kuinoa Leicester City msaidizi wake Thierry Henry, apewe mikoba hiyo,” alisema mtoa taarifa.

Kocha Puel ilikuwa atimuliwe mwishoni mwa msimu ulipita kwani chini yake timu ilifanya vibaya katika mechi saba za mwisho ilishinda mchezo mmoja pekee.

Alisema kuwa bodi ya Leicester, inamtizamia Puel ndani ya mechi tano au sita za mwanzoni mwa Ligi na kama hatapata ushindi bila shaka mkataba wake utachanwa na yeye kuondolewa.