Mara Paa! Msuva atupwa kwa Yanga

Muktasari:

Mafanikio makubwa kwa Yanga ilipocheza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika 1998

Utamu wa vita ni kumjua adui yako, Yanga inajiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza mwakani mmoja wa wapinzani wake katika kusaka taji hilo ni mshambuliaji wake wa zamani, Simon Msuva anayecheza Difaa El Jadidi ya Morocco.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linataraji kutangaza ratiba ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika Jumatano ijayo Desemba 13 jijini Cairo, Misri kwa michuano hiyo itakayoanza mwanzoni mwa Februari na kumalizi Novemba mwakani bingwa atajinyakulia dola 2.5 milioni.

Yanga chini ya kocha, George Lwandamina imedhamiria kufanya vizuri katika michuano hiyo na tayari imeanza kufanya usajili wachezaji mbalimbali wa kimataifa ili kutimiza lengo hilo.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara, Yanga itaanza Ligi ya Mabingwa hatua ya awali kama ilivyokuwa kwa Difaa El Jadidi inayoshiriki mashindano hayo kwa mara kwanza tangu 2010 ilipotolewa katika raundi ya kwanza.

Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani hatua ya makundi itashirikisha timu 16, zitakazogawanywa katika makundi manne, kutokana na mabadilino hayo Yanga inaweza kupata nafasi ya kucheza dhidi ya Msuva katika hatua ya awali, au raundi ya pili kama siyo hatua ya makundi.

Msuva amekuwa katika kiwango kizuri tangu Julai 28, 2017, alipotua Difaa El Jadidi akifanikiwa kufunga jumla ya mabao 15 katika mechi zote. Msuva amefunga mabao tisa katika mechi 13 za kirafiki, mabao mawili katika Kombe la Mfalme katika Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’ amefunga mabao 4, katika mechi 10.

Akizungumzia ratiba hiyo Msuva alisema sitamani tupangwe dhidi ya Yanga hata kidogo, lakini ikitokea hivyo nitawajibika kuipigania Difaa.

“Ukweli ni kwamba Yanga ni timu yangu, imenilea mpaka kufikia hatua ya kuhitajika na timu kadhaa kubwa barani Afrika, lakini Difaa nipo ni kazi si kingine.

“Pamoja na huku, lakini nimekuwa nikiwasiliana mara kwa mara na wachezaji wa Yanga, hii inaonyesha namna gani ambavyo bado ni kama nipo Yanga vile, ndiyo maana nikatangulia kusema sitamani tupangwe pamoja.

“Ila yote kwa yote ya uwanjani yatabakiwa kuwa ya uwanjani na sidhani kama yataharibu mahusiano yangu na Yanga, naipenda sana Yanga na itabaki kuwa timu yangu,” alisema Msuva.

Mbali ya Diffa El Jadidi timu nyingine zitakazokuwa kikwazo kwa Yanga katika kufuzu kwa hatua ya makundi pamoja na ubingwa ni mabingwa watetezi, Wydad Casablanca ya Morocco, mabingwa wa kihistoria Al-Ahly, na Misr Lel-Makkasa (zote za Misri).

Miamba mingine kiboko ya Yanga katika mashindano hayo ni Esperance de Tunis na Etoile du Sahel (Tunisia), kutoka DR Congo ni TP Mazembe na AS Vita Club wakati Algeria imetoa timu za ES Setif na MC Alger.

Afrika Kusini inawakilishwa na Bidvest Wits na Mamelodi Sundowns wakati Sudan watakuwa na timu za Al-Hilal, Al-Merrikh.

Naye kocha wa Yanga, Lwandamina akizungumza na gazeti dada la Mwanaspoti alisema: “Nimeziona hizo timu nazifahamu si kwa kubahatisha ni timu ngumu, lakini ubora wao zaidi unatokana na nguvu ya fedha wanayotumia kufanya maandalizi yaliyobora kabla ya mashindano.

“Najua tutashindana nao japo sijajua tutakutana na timu zipi ila katika maandalizi ni bora tukaangalia kwa ujumla washindani wetu, tunahitaji kuangalia upana na ubora wa kikosi chetu nafikiri hapa ndiyo kwenye kazi,” alisema Lwandamina.

Kama Yanga itapagwa kwenda Ivory Coast itacheza dhidi ya ASEC Mimosas au Williamsville AC.

Kutoka Zambia kutakuwa na ZESCO United na Zanaco wakati Congo kutakuwa na timu za AC Leopards, na AS Otoho. Mali watawakilishwa na timu za Stade Malien na AS Real Bamako huku Nigeria ikiwa na timu za Plateau United, na MFM.

Mbali ya miamba hiyo Yanga anatarajia kupata ushindani mkubwa wa kufuzu kwa hatua ya makundi kutoka kwa Eding Sport ya Cameroon, Al-Tahaddy (Libya), Aduana Stars (Ghana), 1º de Agosto (Angola), Saint George (Ethiopia) na Township Rollers (Botswana).