Manji achimba mkwara Yanga

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji

Muktasari:

Manji aliye chini ya ulinzi wa Polisi kutokana na sakata la kudaiwa kuhusishwa na dawa za kulevya amelazwa katika Hospitali ya JKCI Muhimbili akipatiwa matibabu ambapo alitembelewa na wachezaji wake na kuchimba mkwara huo.

MWENYEKITI wa Yanga Yusuf Manji bado yuko Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akipatiwa matibabu ya moyo lakini akapokea ugeni maalum kutoka kwa manahodha wa timu hiyo na makocha na akawasisitiza wahakikishe wanapambana mwanzo mwisho wala ishu yake isiwapotezee muda.

Waliomtembelea juzi jioni mara baada ya kutua nchini wakitokea Comoro kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kiongozi na muwakilishi wa wachezaji ndani na nje ya uwanja, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msaidizi wake Haruna Niyonzima.

Manji amelazwa Muhimbili katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete akifanyiwa uchunguzi baada ya kujisikia vibaya wakati akiwa Kituo Kikuu cha Polisi kilichopo ufukweni pembeni kidogo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam kilomita chache kutoka Ikulu ya Tanzania.

Ingawa ilikuwa ni mchakato mgumu kwa manahodha wao kumuona bosi lakini walifanikiwa kuwawakilisha wenzao na kumpa pole Manji kwa muda maalum kabla ya kutakiwa kuondoka.

Niyonzima ambaye ni raia wa Rwanda inayotafuta kocha mpya wa timu yao ya Taifa, alisema katika kuonana kwao na Manji walishangazwa na ujasiri wake na aliwaambia matatizo anayoyapitia sasa yasiwahusu kwa namna yoyote bali wanachopaswa kufanya ni kupiga kila anayekuja mbele yao kwa bao za kutosha.

Niyonzima alisema Manji aliwaambia kwamba amesikia ushindi mkubwa walioupata wa mabao 5-1 dhidi ya Ngaya ya Comoro na kuwapongeza kwa hatua hiyo na sasa waongeze dozi bila kujali kinachoendelea katika maisha yake.

Aidha Niyonzima na Cannavaro walimhakikishia Manji kwamba ushindi wao dhidi ya Ngaya ni zawadi kwake kumfariji na matatizo aliyonayo na wataendelea kupambana kuhakikisha wanashinda mechi zao zote.

“Tulishindwa kwenda majumbani kusema ukweli, tukawaomba viongozi watupeleke tukamuone mwenyekiti (Manji) na tukapata hiyo nafasi ingawa tulipewa muda mfupi ulitosha kabisa kukata kiu yetu na alitushangaza alipotuambia anajua yuko katika matatizo lakini sisi wachezaji tunatakiwa kuendelea na mapambano kuhakikisha timu haifanyi vibaya,” alisema Niyonzima ambaye huvaa jezi namba nane uwanjani na hajawahi kuifunga Simba licha ya kwamba siyo straika.

“Amesema yuko katika matatizo na anaamini kama yalivyoanza pia yataisha na Mungu akisaidia atarudi katika majukumu yake na hataki eti kwa kuwa yuko katika matatizo iwe nafasi ya timu kufanya vibaya, akatupongeza kwa ushindi na tumemuahidi tutajituma kwa kutafuta ushindi ili tumfariji katika kipindi kigumu anachopitia,”alisema Niyonzima ambaye ana watoto wanne wakike watatu na wa kiume mmoja.

MWAMBUSI

AFUNGUKA ZAIDI

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema: “Unaona mechi zilivyo karibu sasa kuepuka ugumu ni lazima tufanye vizuri mechi za kwanza ili mchezo wa marudiano tusitumie nguvu nyingi hili litatusaidia sana.”

“Tuna majukumu mengi ratiba inaonyesha kwamba tunapocheza tunarudiana siku chache baadae, lazima tuwe makini, tunataka kufanya makubwa ndiyo maana tunabadili mambo,”alisisitiza kocha huyo wa zamani wa Mbeya City.

Yanga na Ngaya zitarudiana Jumamosi hii Uwanja wa Taifa na mwamuzi ni Alex Muhabi wa Uganda. Yanga ikivuka kwenye mchezo huo itacheza na mshindi kati ya APR na Zanaco kwenye mechi itakayopigwa Kigali, Rwanda baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa awali pale kigali.

Nahodha msaidizi wa APR, Michel Rusheshangoga ametamba kwamba kazi waliyonayo kwa Zanaco ni nyepesi sana wala haiwaumizi kichwa kama ambavyo wangefungwa au kuruhusu bao kwenye mchezo wa kwanza waliokuwa ugenini.

APR anatakiwa kushinda ili asonge mbele lakini sare yoyote ya magoli itamtoa.