Manara: Mabadiliko hayaepukiki Simba

Saturday August 12 2017

 

By Fredrick Nwaka,Mwananchi fnwaka@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Simba ikitarajia kufanya mkutano wake mkuu wa kawaida kesho Jumapili, Ofisa Habari Haji Manara amesema mabadiliko katika uendeshaji wa klabu hiyo hayaepukiki licha ya baadhi ya wanachama kujaribu kuyazuia.

Wiki iliyopita mwenyekiti wa baraza la Wadhamini, Khamis Kilimoni alifungua kesi mahakamani kupinga mkutano huo ambao mbali na agenda za mapato na matumizi utapitia mchakato wa kubadili uendeshaji wake.

 Manara alisema wazee waliofungua kesi hawana budi kufikiria mara mbili hatima ya klabu hiyo.

"Tunaishukuru mahakama kwa kutenda haki kuruhusu mkutano ufanyike, lakini tunamuomba mzee wetu aondoe kesi mahakamani kwa kuwa ni kinyume na katiba ya klabu na pia ni kinyume na katiba ya TFF,"alisema Haji.

Aliingeza kuwa Simba haiwezi kung'ang'ania mfumo wa zamani ambao hauwezi kuisaidia kupiga hatua.

"Hatuwezi kuishi enzi za miaka ya 70 wazee wetu waje kwenye mkutano na mwisho wa siku kila mwananchama ana haki,"alisema

Mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere kuanzia saa 4 asubuhi ambapo Haji aliwataka wanachama kuwahi kabla ya muda huo ili kuhakiki taarifa zao.

Mkutano huo wa Simba ni mwendelezo wa agenda ya kubadili mfumo wa uendeshaji kuwa wa hisa ambapo tayari mfanyabiashara Mohammed Dewji ameonyesha nia ya kuwekeza Sh. 21 bilioni kwa kununua hisa asilimia 51.