Manara: Awamu hii Rais Magufuli atatuita mwenyewe

Dar es Salaam.Baada ya kutia aibu mbele ya a Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, wakichapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bar, Simba imepania kufanya makubwa msimu mpya wa 2018/19.

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kitendo cha kufungwa mbele ya rais kilizua utani mwingi kwamba tulimwita wenyewe halafu tunaabika wenyewe, ngoja tuchukue ubingwa wa kimataifa ili atuite mwenyewe Ikulu kutupongeza.

“Naomba niweke wazi kuwa Simba ina kikosi bora ambacho kinaweza kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na nje ya nchi," alisema Manara.

Manara alisema hawatakuwa na nafasi ya kutoa mwaliko kwa Rais zaidi yeye mwenyewe atawapa mwaliko wao kutokana na kutimiza kile alichowaeleza mara baada ya kuwa kabidhi kombe ambapo aliwataka wafanye vizuri kimataifa ili kuitangaza nchi.

Katika hatua nyingine alizungumzia tamasha la Simba Day, Manara amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kushudia mechi dhidi ya Asante Kotoko mchezo huo utakua maalumu kwaajili ya kutambulisha wachezaji wao pamoja na jezi zao mpya.

"Simba ina kikosi bora naamini mashabiki wataujaza uwanja kwa lengo la kuja kushuhudia kikosi chao kilivyofanya maandalizi mazuri kuelekea msimu mpya wa Ligi na mashindano ya Ligi ya Mabingwa, katika tamasha hilo kutakuwa na utangulizi wa michezo mbalimbali ambapo Dodoma FC watacheza dhidi ya Simba ," alisema.

Pia, alisema mara baada ya tamasha lao hilo wataanza mipango ya ujenzi wa Uwanja wao wa Bunju ambao wanatarajia kuanza kuutumia kwaajili ya maandalizi na kuweka wazi kuwa wataanza na nyasi asili kutokana na nyasi zao za Bandia kuwa kama ushahidi kwa viongozi wao wanaoshikiliwa.