Man Utd, Barca, Chelsea kuwasha moto Ulaya

Muktasari:

England ipo katika nafasi nzuri ya timu zake zote kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa

Manchester, England.Hakuna namna nzuri ya Manchester United kutinga hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa ushindi mtamu dhidi ya CSKA Moscow huko Old Trafford usiku wa leo Jumanne.

Man United ilijichelewesha yenyewe kufuzu hatua hiyo ya 16 bora, baada ya kukubali kichapo kutoka kwa FC Basel kwenye mechi yao iliyopita huko Uswisi. Lakini, kwa Man United kushindwa kufuzu hatua inayofuata, basi itakuwa maajabu ya mwaka kwa hali ilivyo kwa sasa.

Wababe hao wanaonolewa na Jose Mourinho wamekusanya pointi 12, tatu zaidi ya CSKA na Basel - ambazo zote zitacheza mechi zao za mwisho usiku wa leo. Ipo hivi, kama Basel wataichapa Benfica kisha Man United ikachapwa na CSKA, basi kitakachotazamwa ni matokeo ya timu hizo tatu.

 Kwa hali ilivyo kwa sasa, Man United ndiyo wanaokontroo kundi hilo. Man United watatupwa nje kama tu watapigwa saba na CSKA Old Trafford, zaidi ya hapo wataendelea kuongoza kundi lao hata watapoteza kwa idadi ya mabao yasiyozidi manne.

 Kwa CSKA kufuzu basi ni kuomba washinde mechi yao na kisha Basel wakashindwa kupata ushindi mbele ya Benfica, ambao hawajashinda mechi hata moja.

Zaidi ya hapo, CSKA watafuzu kama tu, watashinda zaidi ya mabao matatu huko Old Trafford kisha Basel watashinda. Lakini, si hadi wapate ushindi Old Trafford? Kuwazuia Man United wasiingie hatua hiyo ya mtoano utakuwa muujiza, kwa sababu wao wanahitaji pointi moja tu, kuvuka na kuongoza kundi.

Kibarua kingine cha mikikimikiki hiyo kitaikabili Chelsea wataokuwa kwenye vita ya kuongoza kundi dhidi ya AS Roma. Chelsea wao wenye pointi 10 watacheza na Atletico Madrid uwanjani Stamford Bridge, wakati Roma na pointi zao nane watakuwa nyumbani pia kucheza na Qabarag.

Atletico wenye pointi sita wao watafuzu kama tu watashinda 3-0 kwa Chelsea na kisha Roma washindwe kupata ushindi mbele ya Qabarag.

Vigogo wengine wa England watakaokuwa kwenye vita ya kuongoza kundi ni Tottenham ambao na pointi zao 13 kesho, Jumatano watakuwa na kibarua mbele ya APOEL huko Wembley, huku Real Madrid wenye pointi 10 watakuwa na shughuli dhidi ya Borussia Dortmund huko Bernabeu. Sare tu itawatosha Spurs kuongoza kundi lao.

Liverpool nao watakuwa kwenye vita ya aina hiyo ambapo, wakiwa na pointi zao tisa watacheza dhidi ya Spartak Moscow huko Anfield, wakati wapinzani wao kwenye vita hiyo, Sevilla wenye pointi nane watakuwa ugenini kwa Maribor.

Spartak watafuzu kama wataishinda Liverpool na Sevilla wakakwama huko Maribor. Manchester City wao wameshafuzu.

RATIBA YA MECHI NYINGINE

Leo, Jumanne

Olympiakos        v Juventus         

Barcelona            v Sporting CP                    

Celtic                     v Anderlecht                     

Bayern Munich v PSG                   

 

Kesho, Jumatano

RB Leipzig            v Besiktas                           

Porto                     v Monaco                                           

Shakhtar Donetsk            v Man City          

Feyenoord                          v Napoli