Man United inaongoza kwa wagonjwa Top Six

MANCHESTER, ENGLAND. KWA misimu mitatu iliyopita, timu za Top Six kwenye Ligi Kuu England tofauti ya viwango vyao ndani ya uwanja ilikuwa kwenye timu kuwa na bahati ya kutokuwa na majeruhi wengi.

Msimu uliopita, Chelsea ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu England wakiwatesa wapinzani wao kwa kuweza kuchezesha kikosi kile kile cha kwanza karibu kila wiki kwa kuwa hakuwa na majeruhi wengi na hawakuwa na michuano mingi pia.

Kilikuwa kitu kizuri kwa Kocha Antonio Conte, kwa sababu karibu msimu wote kikosi chake kilibaki kilekile na hatimaye kunyakua ubingwa.

Makala haya hayahusu timu iliyokabiliwa na majeruhi mara nyingi katika Ligi Kuu England kwa upande wa vigogo wa Top Six.

Chelsea, majeruhi 98

Tangu mwanzoni mwa msimu wa 2014/15, kwenye orodha ya timu za Top Six, Chelsea ndiyo timu iliyopata majeruhi mara chache zaidi kuliko timu yoyote kwenye Ligi Kuu England.

Timu hiyo imekumbwa na majeruhi mara 98, huku kwa ujumla wachezaji wake wakiwa nje ya uwanja kwa siku 1,499.

Majeraha yanayosumbua zaidi ni goti, ambapo wachezaji wake waliopata tatizo hiyo wamekuwa nje ya uwanja kwa jumla ya siku 289.

Tottenham, majeruhi 124

Kwa msimu hiyo mitatu, Tottenham Hotspur imekuwa ikifanya vizuri Ligi Kuu England na kufanikiwa kushika nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Jambo hilo limedaiwa kutokana na kutokuwa na majeruhi mara nyingi kwenye kikosi chake, ambapo kwa muda wote huo, Spurs imeshuhudia majeruhi mara 124, huku ikiwakosa wachezaji wake kwa siku 2,751.

Majeraha yanayosumbua ni enka, na imeshuhudiwa wachezaji wakiwa nje ya uwanja kwa siku 710.

Man City, majeruhi 146

Vijana wa Kocha Pep Guardiola, Manchester City kwa sasa wanapepea tu kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England baada ya kushinda mara 10 na kutoka sare moja tu katika mechi 11 ilizocheza kwenye ligi hiyo hadi kufika sasa.

Rekodi zao za majeruhi kwa kipindi cha misimu mitatu zinaonyesha kwamba Man City imeshuhudia wagonjwa kwenye kikosi chake mara 146, jambo lililowafanya kuwakosa mastaa wake kwa jumla wake kwa kipindi cha siku 2,795.

Misuli ya nyuma ya paja ndiyo majeraha yanayosumbua zaidi Man City na imeshuhudia wakali wake wakiwa nje ya uwanja kwa siku 571.

Arsenal, majeruhi 147

Kwa muda mrefu, tatizo kubwa ambalo limekuwa likisumbua Kocha Arsene Wenger kwenye kikosi chake ni majeruhi, huku akiwakosa wachezaji wake muhimu kwa muda mrefu wakiwa nje ya uwanja.

Katika kipindi cha misimu mitatu, Arsenal imeshuhudia wagonjwa kwenye kikosi chake mara 147, huku wachezaji walioumia kwa jumla wake wakikosa kuitumikia timu yake katika kipindi cha siku 4,131 na kumpa wakati mgumu kocha Wenger.

Goti ndiyo majeraha makubwa yanayosumbua mastaa wa Arsenal na kuwafanya wawe nje ya uwanja kwa siku 483.

Liverpool, majeruhi 162

Waathirika wengine wakusumbuliwa na orodha ndefu ya majeruhi kwenye kikosi chao ni Liverpool.

Wababe hao wa Ligi Kuu England wameshuhudia majeruhi mara 162 kwenye kikosi chao huku wachezaji walioumia wakishindwa kutoa huduma kwenye timu hiyo kwa jumla ya siku 4,153 wakiwa nje ya uwanja kwa kuwa wagonjwa.

Jambo hilo limedaiwa kuigharimu kwa kiwango kikubwa Liverpool katika kasi yake ya kuukimbizia ubingwa wa England.

Majeraha ya goti ndiyo yanayosumbua huko Anfield na mastaa wake wamekosa mechi kwa siku 607.

Man United, majeruhi 187

Kwenye orodha ya Top Six Ligi Kuu England, Manchester United ndio wanaoongoza kwa kushuhudia majeruhi mara nyingi katika kikosi chake baada ya kupata wagonjwa mara 187 katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita.

Idadi hiyo ya majeruhi imewafanya Man United kukosa huduma ya wachezaji wake muhimu kwa siku 4,096 wakiwa nje ya uwanja kutokana na kuugua na hivyo kuongeza ugumu katika kufanya vizuri.

Mastaa wengi wa Man United wamekuwa wakisumbuliwa na maumivu ya enka, ambapo wagonjwa wa maradhi hao wamekuwa nje ya uwanja kwa siku 492.