Mambo haya kuikoa Yanga

Muktasari:

Ipo hivi; Mashabiki bado wanaugulia maumivu ya chama lao kuchapwa 4-0 na Gor Mahia kule Kenya na jana Ijumaa wachezaji wamegoma kufanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano, lakini baadhi ya wachezaji na viongozi wa zamani wameibuka na kutoa mwongozo wa namna bora ya kuikoa timu ili isipoteze mwelekeo kabisa.

KAMA ndio kupambana na hali zao basi Yanga wanapata tabu sana kwa sasa. Huku tetesi za kujiuzulu kwa viongozi wake akiwamo Katibu Mkuu, Charles Mkwasa na Ofisa Habari, Dismas Ten, zikiendelea kuwavuruga wanachama na mashabiki, mengine mapya yameibuka.

Ipo hivi; Mashabiki bado wanaugulia maumivu ya chama lao kuchapwa 4-0 na Gor Mahia kule Kenya na jana Ijumaa wachezaji wamegoma kufanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano, lakini baadhi ya wachezaji na viongozi wa zamani wameibuka na kutoa mwongozo wa namna bora ya kuikoa timu ili isipoteze mwelekeo kabisa.

Wachezaji hao wamegoma kushiriki kwenye programu ya mazoezi iliyopangwa kuanza jana Uwanja wa Polisi Kurasini, kwa kile kinachodaiwa kushinikiza kulipwa mishahara na fedha za usajili.

Yanga pia imekuwa ikipambana kumalizana na wachezaji wake nyota kama Kelvin Yondani, Hassan Kessy na Andrew Vicent (Dante) ambao mpaka sasa hawajasaini mikataba mipya, wakitaka kwanza kulipwa mabaki ya fedha za usajili uliopita ndipo wamwage wino tena.

Awali, benchi la ufundi la Yanga lilipanga jana ndio lianze programu kwa ajili ya kujipanga kulipa kisasi dhidi ya Gor katika vumbi la hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini limelazimika kuvunja mazoezi kutokana na kundi kubwa la wachezaji kuingia mitini.

Habari zinaeleza kuwa ukiondoa maofisa wa benchi la ufundi, wachezaji waliofika mazoezini ni watatu tu; Deus Kaseke, Mrisho Ngassa na Heritier Makambo ambao wote ni wapya waliosajiliwa hivi karibuni.

“Suala la kudai ni kweli tunaidai klabu tena fedha nyingi, lakini binafsi sikuhudhuria mazoezi leo (jana) asubuhi kwa sababu sijisikii vizuri kimwili,” alisema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe.

Mwanaspoti liliwasiliana na Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, ambaye alikiri kuvunja programu ya mazoezi yaliyotakiwa kufanyika jana kutokana na wachezaji kutohudhuria.

“Ni kweli leo (jana) tulikuwa na programu ya mazoezi, lakini walikuja wachezaji wachache sana na wengine hawakuonekana, hivyo tulishindwa kuendelea. Nimepewa taarifa kuwa hawakufika kwa sababu wanadai mishahara,” alisema Zahera.

Lakini, wakati hayo yakiendelea aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako alisema kinachoigharimu timu hiyo kwa sasa ni mwingiliano wa madaraka. Amesema ndani ya Yanga sasa hivi kila mtu anajiona yuko juu ya mwingine.

“Kwa kawaida Katibu ndiye mtendaji mkuu wa klabu, nilichokiona zipo baadhi ya kamati zinazoingilia utendaji wake na hilo ndilo jambo lililomfanya Mkwasa ajiweke kando,” alisema.

“Nawashauri Wana Yanga huu si wakati wa malumbano, bali uwe wa kutengeneza ili kupatikane wachezaji makini, la sivyo kinachokuja mbele kitakuwa na maumivu makali kuliko haya.”

Naye mchambuzi mahiri wa soka nchini na mchezaji wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars, Ally Mayay, amewataka wanachama wa klabu hiyo kutambua umuhimu wa Mkwasa kuwa ni mtu aliyecheza soka na pia kufundisha, hivyo anaweza kuwafaa kuliko mwingine kwa sasa.

“Migogoro ya uongozi Yanga kama itaendelea hivyo, msimu mpya Yanga itafanya vibaya kuliko wakati wote ambao imewahi kushiriki ligi, Hapa ni lazima kutumia busara ili kumaliza matatizo ndani ya klabu kisha mambo ya usajili yaendelee,” alisema.

Straika wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, alisema mpaka sasa hajaona mchezaji wa maana aliyesajiliwa na chama lake hilo, hivyo akashauri tofauti za uongozi ziwekwe kando kwanza ili timu isipoteze mwelekeo.

“Hali halisi Yanga ni mbaya, hivyo kila mwana Yanga ambaye anapenda maendeleo asiwe sehemu ya matatizo, yote haya yamekuja baada ya kuondoka kwa Manji (Yusuf),” alisema.

Kuhusua kuachia ngazi kwa Ten, ambako taarifa zilianza kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii, mwenyewe aliibuka na kukanusha akidai bado yupo na watu wapuuze taarifa hizo.