Mama Uwoya:Simpendi Dogo Janja, hana adabu

Muktasari:

Oktoba 28 mwaka jana Dogo Janja(23) na Uwoya(29) walifunga ndoa ya siri ilizua gumzo kutokana na kuwepo kwa utofauti mkubwa wa umri kati yao.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Irene Uwoya kusema ameshindwa kumpeleka Dogo Janja kwa mama yake kutokana na kuwa mtu wa kusafiri, mama yake Neema Mrisho amesema hampendi msanii huyo kwa kuwa hana adabu.

Akizungumza na MCL Digital leo, Machi 19, mama Uwoya amesema hata wangeamua kwenda kujitambulisha asingewapokea kwa kuwa mwanaume huyo aliyemuoa mtoto wake hana adabu na ndio maana ameweza kufunga ndoa bila hata kufuata taratibu.

Akihojiwa mwishoni mwa wiki na kituo cha redio Clouds, Uwoya alisema pamoja na kufunga ndoa tangu Oktoba mwaka jana, hajampeleka Dogo kwa mama yake kwani amekuwa mtu ambaye anasafiri mara kwa mara huku akiahidi kuwa siku moja wataenda.

Akizungumzia hilo, mama Uwoya amesema utetezi huo hauna mashiko kwani hata kama anasafiri hawezi kusafiri mwaka mzima, isipokuwa ukweli ni kwamba mtoto wake anajua wazi kwamba ndoa hiyo hawaitambui na pia hawamkubali Dogo kwa kuwa ni mtoto ambaye hana adabu.

“Yaani ndugu mwandishi sijui nisemaje na mambo haya sipendi sana kuyaongea kwenye media kwa kuwa haipendezi kubishana na mtoto uliyemzaa kwenye vyombo vya habari kwani mwisho wa siku yule ni mtoto wetu tu pamoja na kufanya mambo ambayo hayajatupendeza, lakini muelewe kwamba ndoa hiyo sisi kama wazazi hatuitambui na hatutaitambua,”alisema mama huyo.

Hata hivyo mama Uwoya alienda mbali zaidi na kudai kwamba ndoa hiyo ibaki kutambuliwa na hao Irene aliowaita kuwa ni ndugu zake walioenda kushiriki harusi yake na hao waliomfungisha ndoa kwani pamoja na wao kuwa Dar es Salaam, lakini wanashangaa walijitokeza ndugu ambao hawawajui katika kusimamia jambo hilo.

“Siku ambayo ndoa inafungwa ndugu zake na wazazi wake tulikuwepo, lakini tulishangaa kuona kwenye mitandao kuwa amefunga ndoa na hata ilipozidi kuvuma na kumuuliza majibu yake ilikuwa kwamba alikuwa anacheza movie,  hivyo tuliamua kuachana nalo kwani huwezi kumlazimisha mtu akuambie ukweli kwa kile anachokiamini yeye.”

Mbaya zaidi alisema Uwoya alifanya jambo hilo akiwa anajua wazi kwamba ana mume halali ambaye hawajawahi kupeana talaka, hivyo kama wazazi wasingeweza kulipokea jambo hilo na kuongeza kwamba walifuatilia hadi Rita kujua kama kuna talaka ilishatolea lakini hawakukuta jambo hilo.

Alipoulizwa kama atakuwa tayari kumpokea Dogo kwa sasa baada ya Ndikumana kufariki, mama huyo aliendelea kukaza akisema hawezi kufanya hivyo kwani alishawakosea adabu tangu mwanzo hivyo kwao amekosa sifa ya kuwa mkwe wao.

Oktoba 28 mwaka jana Dogo Janja(23) na Uwoya(29) walifunga ndoa ya kimya kimya ambayo ilizua gumzo kutokana na kuwepo kwa utofauti mkubwa wa umri kati yao.

Hata hivyo kwa kipindi chote hicho tangu waoane, Dogo Janja ndiye aliyekuwa muwazi kuzungumzia suala hilo, huku Uwoya akiwa anakwepakwepa mpaka pale walipoonekana kwa mara ya kwanza pamoja katika harusi ya Shilole.