Malinzi ajitwisha zigo la Zahoro Pazi

Muktasari:

Malinzi jana Jumatatu alikutana na Pazi ili kusikiliza malalamiko yake ya kuzuiwa kwa ITC yake na klabu ya FC Lupopo, ambapo kikao hicho kiliwahusisha pia baba mzazi wa Pazi, Idd Pazi ‘Father’ na mwakilishi wa Mbeya City, Mohammed Mashango.

STRAIKA wa zamani wa Simba na Azam, Zahoro Pazi amesajiliwa Mbeya City ikiwa ni baada ya misimu karibu miwili akishindwa kuzitumikia timu zinazomsajili kwa kukosekana Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Hata safari hii akiwa ametua Mbeya kulikuwa na hofu ya kushindwa kuitumikia timu hiyo kwani ITC yake imezuiliwa na Klabu ya FC Lupopo ya DR Congo, lakini Rais wa TFF, Jamal Malinzi ameamua kujitosa ili kumsaidia mtoto huyo wa kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Idd Pazi.

Malinzi jana Jumatatu alikutana na Pazi ili kusikiliza malalamiko yake ya kuzuiwa kwa ITC yake na klabu ya FC Lupopo, ambapo kikao hicho kiliwahusisha pia baba mzazi wa Pazi, Idd Pazi ‘Father’ na mwakilishi wa Mbeya City, Mohammed Mashango.

Pazi amekuwa akilalamika kutolewa kwa ITC yake bila ya kufanya makubaliano na Lupopo iliyong’ang’ania hati hiyo, huku lawama zake akizielekeza kwa mmoja wa maafisa wa juu wa shirikisho hilo (jina kapuni).

Wiki iliyopita, mchezaji huyo aliwasiliana na Malinzi ili kumuomba aingilie kati katika kuhakikisha ITC yake inapatikana na hatimaye aweze kuichezea Mbeya iliyomsajili kwenye dirisha dogo.

Ndipo Malinzi jana aliamua kujitwisha mzigo huo na kuonana na mchezaji huyo ili kuona namna ya kumsaidia, ambapo baba mzazi wa Pazi, alithibitisha kikao hicho ambacho hatma ya mchezaji huyo ipo mikononi mwake kwa sasa.

“Tunashukuru Rais Malinzi ameelewa na ametuahidi kutusaidia ndani ya siku saba, amesema atasimamia mwenyewe kwani amegundua wapi kuna tatizo ndani ya shirikisho lake. Malinzi amemruhusu Zahoro kurudi Mbeya kuendelea na mazoezi na huenda mechi ijayo akacheza,” alisema Father.

“Kinachoonekana ni kwamba kuna mchezo ulichezwa kati ya kiongozi mmoja wa TFF kwa kutoa barua feki na kufoji sahihi ya mchezaji wakitumia saini yake ya zamani akiwa Simba, ila kikubwa tunamwachia Rais atusaidie tu mtoto acheze,” alisema Father.

Mwanaspoti inafahamu kuwa Pazi amemuomba Malinzi amsaidie kupatiwa hata kibali cha muda ili aendelee kucheza kuokoa kipaji chake huku akishughulikia kurejeshwa kwa ITC yake kutoka Congo.