Malinzi, Kaburu na Wambura watikiswa

Muktasari:

Kwa kauli hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja, ni wazi sasa vigogo wanaowania nafasi za juu za shirikisho hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa.

BARAZA la Michezo Tanzania (BMT), juzi Jumanne lilitangaza kwamba wagombea katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ambao wanaongoza katika vyama vingine vya soka wanapaswa kuachia ngazi sehemu moja endapo watapata uongozi katika shirikisho hilo.

Kwa kauli hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja, ni wazi sasa vigogo wanaowania nafasi za juu za shirikisho hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa.

Wagombea walijitokeza katika nafasi ya Rais na Makamu wake ambao wanaguswa na taarifa ya BMT ni Rais Jamal Malinzi anayetetea nafasi yake ambaye atapaswa kuachia nyadhifa ya Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera ambayo anaishikilia hadi sasa.

Wengine wanaoguswa ni Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, ambaye amechukua fomu kimya kimya.

Katika nafasi ya Makamu wa Rais, wagombea Mulamu Nghambi, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Michael Wambura nao watalazimika kuachia madaraka ya uenyekiti wa vyama vyao vya mikoa.

Nghambi yeye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Dodoma, Kaburu anaongoza mkoa wa Pwani, wakati Wambura ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara.

Kanuni ya 8(1) na (2) ya BMT ndiyo inayowabana wagombea hao. Kanuni hiyo inawataka Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi na Mweka Hazina kuwa hawaruhusiwi kushika nafasi za uongozi zaidi ya moja kwenye vyama tofauti vinavyoshughulikia aina moja ya mchezo.

Hata hivyo mpaka sasa Katiba ya TFF inawaruhusu viongozi wa ngazi ya juu kushika madaraka hayo kwa maana ya kuongoza vyama vya mikoa ama klabu, hivyo baada ya uchaguzi huo watapaswa kufanya marekebisho ya Katiba ili kuendana pia na kanuni za BMT