Makonda kunogesha Simba na Arusha United

Arusha: Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa kirafiki kati ya Simba Sc na Arusha United utakaochezwa leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.

 Msemaji wa timu hiyo Haji Manara alisema wanatumia michezo ya kirafiki kwaajili ya kukiimalisha kikosi hasa katika michezo ya mikoani ili kuzoea viwanja kabla ya ligi kuanza kwa kuwa michezo mingi itakuwa wakitoka nje ya Mkoa.

 “tumefarijika kufika Mkoani hapa kwani wachezaji wengi watakuwa wanajifunza vitu tofauti wanapokutana na wachezaji wa ligi za daraja la chini kwani mwishoni mwa wiki iliyopita tulijifunza pia tulipokutana na Namungo Fc” alisema Manara.  

 Kwa upande wake Nahodha wa timu ya Simba John Bocco amesema kuwa michezo ya kirafiki inasaidia kuwajenga zaidi lakini kuwataka Arusha kutumia ujio wao kama fursa ya kuchangamkia fursa ya kupambania timu zao kufuzu hatua ya kucheza ligi kuu

 “Arusha hakuna timu ya ligi kuu hivyo watu wa Arusha waje kwa wingi kuona timu zao zinavyocheza na wazisapoti ili kufanikisha mwakani kupata burudani ya ligi kuu maana ni aibu mkoa kama huu wa kitalii na kusifika kibiashara hakuna burudani ya soka”

 Kocha Mkuu wa timu hiyo Fredy Felix “Minziro” alisema baada ya kucheza na Simba watakuwa na mchezo mwingine na timu inayoshiriki ligi kuu hii yote kutokana na mahusiano mazuri aliyonayo kwa viongozi wa timu.

 “hatutaangalia kufungwa, bali matokeo yoyote tutayapokea na hapo ndio tutakuwa tunaanzia katika harakati za kujirekebisha na kupanga kikosi changu” alisema Minziro.

 Viingilio katika mchezo huo vitakuwa 20,000 VIP A’, 10,000 VIP B’ na 5,000 kwa mzunguko huku mlezi wa timu ya Arusha United Mrisho Gambo alisema lengo ni kuona wanapata changamoto kabla ya kuanza kwa ligi daraja la kwanza (FDL) tutakaposhiriki.

 "Wengi wanautazama Mkoa wa Arusha kwa jicho la kipekee hasa kwenye michezo kwa kukosa timu ligi kuu lakini hivi sasa tiumejipanga kurejesha heshima kwenye Mkoa wetu kwa kushirikiana wadau wote kuwa na sauti moja" alisema Gambo.