Makocha walipiga pesa ndefu za fidia za kufukuzwa kazi

Muktasari:

  • Kama hilo litatokea la Conte kufutwa kazi Stamford Bridge, basi klabu hiyo italazimika kumlipa fidia Mtaliano huyo kwa sababu itakuwa imemtimua kabla ya mkataba wake kufika mwisho.

ANTONIO Conte kwa sasa amekuwa gumzo kubwa huko Chelsea, akidaiwa huenda akawa kocha wa kwanza kufutwa kazi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Kama hilo litatokea la Conte kufutwa kazi Stamford Bridge, basi klabu hiyo italazimika kumlipa fidia Mtaliano huyo kwa sababu itakuwa imemtimua kabla ya mkataba wake kufika mwisho.

Hata hivyo, jambo hilo likitokea halitakuwa mara ya kwanza na Conte hatakuwa kocha wa kwanza kufutwa kazi kisha kulipwa fidia kutokana na jambo hilo kuwakuta makocha wengine kibao.

Hawa hapa makocha waliopiga pesa ndefu kwa kulipwa fidia ya kufutwa kazi kwenye klabu zao.

Andre Villas-Boas (Chelsea, Pauni 12 milioni)

Mreno Andre Villas-Boas (AVB) yalimkuta makubwa Chelsea baada ya kufutwa kazi kutokana na kikosi hicho kufanya vibaya kwenye mechi zake. Baada ya kuwa kwenye kibarua cha kuinoa Chelsea kwa miezi saba tu, AVB alionyeshwa mlango wa kutokea, lakini kwa sababu mkataba wake ulivunjwa, basi kocha huyo alilipwa Pauni 12 milioni kama fidia.

Jose Mourinho (Chelsea, Pauni 10 milioni)

Septemba 2007 ilikuwa awamu yake ya kwanza Kocha Jose Mourinho kufutwa kazi huko klabuni Chelsea. Baada ya kutua kwenye timu hiyo kisha kuipa mataji ya mawili ya haraka, Mreno Mourinho yalimkuta makubwa baada ya kufungiliwa mlango wa kutokea Stamford Bridge kutokana na timu kuwa na mwenendo mbaya kwenye ligi. Hata hivyo, hakuondoka mikono mitupu, kwa kuwa mkataba wake ulivunjwa, akalipwa fidia ya Pauni 10 milioni.

Jose Mourinho (Chelsea, Pauni 10 milioni)

Kocha Jose Mourinho amekumbana na fagio la kufutwa kazi klabuni Chelsea mara mbili tofauti. Baada ya kurudi klabuni hapo kisha kuipa ubingwa mwingine wa Ligi Kuu England, Mourinho alifutwa tena kazi Desemba 2015.

Kabla hajafutwa kazi, Mourinho alikuwa ameongeza mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 30 milioni ambao, ulikuwa unaishia mwaka 2019, hivyo kwa kufutwa kazi, akalipwa fidia ya Pauni 10 milioni.

Kenny Dalglish (Liverpool, Pauni 8.5 milioni)

Kocha Kenny Dalglish alivuna pesa nyingi zaidi wakati alipofutwa kazi klabuni Liverpool katika awamu yake ya pili kuliko hata alipokuwa akiichezea timu hiyo. Baada ya kufutwa kazi Mei 2012, kocha huyo alifutwa kazi na kwa sababu bado alikuwa na mkataba wake huko Anfield ilibidi alipwe fidia ya Pauni 8.5 milioni.

Brendan Rodgers (Liverpool, Pauni 7 milioni)

Oktoba 2015, Brendan Rodgers alikumbana na fagio la chuma Liverpool na kufutwa kazi. Baada ya kikosi hicho kushindwa kufanya vizuri katika soko la usajili, Rodgers alishindwa kutengeneza kikosi matata na matokeo yake kilishindwa kupambana na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu England na safari ikamkuta. Kwa kuwa mkataba wake ulikuwa bado haujafika mwisho, Liverpool ilibidi kumlipa fidia kocha huyo, hivyo alivuna Pauni 7 milioni kwa kufutwa kazi.

David Moyes (Man United, Pauni 4 milioni)

Baada ya kuondoka Sir Alex Ferguson, David Moyes alibamba dili la kuinoa Manchester United. Lakini, kwenye kikosi hicho hakudumu sana kwani hadi kufikia Aprili 2014 alifutwa kazi kutokana na timu kufanya hivyo, kwenye Ligi Kuu England na michuano mingine iliyokuwa ikishiriki.

Kwa sababu Moyes alifutwa kazi kwenye mwaka wa kwanza tu wa mkataba wake klabuni Old Trafford, hivyo ilibidi alipwe fidia ya Pauni 4 milioni. Moyes alikabidhi mikoba kwa Lous van Gaal, ambaye naye alifutwa kazi Old Trafford na nafasi yake kuchukuliwa na Mourinho.

Wakocha wengine waliovuna fidia kubwa kwa kutimuliwa

Kocha Garry Monk aliweka mfukoni Pauni 3 milioni baada ya kufutwa kazi huko Swansea City, Desemba 2015, wakati England ililazimika kumlipa Sven-Goran Eriksson fidia ya Pauni 2.5 milioni wakati ilipomfuta kazi kocha huyo Julai 2014.

Muitaliano Carlo Ancelotti, naye alilipwa fidia ya Pauni 2.5 milioni wakati alipofutwa kazi huko Real Madrid, Mei 2015 sawa na kiasi alicholipwa Rafa Benitez, Desemba 2010 wakati alipofutwa kazi huko Inter Milan baada ya kikosi chake kuchemsha.

Kocha, Fabio Capello alilipwa fidia ya Pauni 1.5 milioni wakati alipofutwa kazi inoa England.