Makambo freshi, Tambwe anatisha

MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kuanza kutabasamu baada ya hati ya uhamisho ya kimataifa ya Mkongo, Heritier Makambo kutua nchini ili kumpa nafasi ya kukinukisha Jangwani, huku Amissi Tambwe akionyesha maajabu yake.

Kutua kwa ITC hiyo ya Makambo, inampa nafasi ya kucheza mechi ya mwisho ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports, huku hati ya kipa Nkinzi Kindoki ikitarajiwa kufika leo Jumanne.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika ndiye aliyefichua ishu hiyo ya Makambo, aliyesajiliwa ili kuziba nafasi ya Obrey Chirwa aliyetimkia Misri.

Katika hatua nyingine, straika Amissi Tambwe katika mazoezi ya jana Uwanja wa SUA mjini hapa alifanya maajabu kwa kugeuka kipa kutokana na kukosekana kwa makipa wa kumsaidia Kindoki. Tambwe alionyesha umahiri kwa kudaka michomo ya washambuliaji wenzake, akichuana na Kindoki.

Makipa Ramadhani Kabwili na Beno Kakolanya hakuwepo kambini kutokana na matatizo binafsi, Beno akifiwa na kaka yake japo jioni ya jana alikuwa njiani kuwahi kambi hiyo ya kujiandaa na mechi ya USM Alger ya Algeria na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.