Makambo awashtua Jangwani

Muktasari:

  • Usishtuke, ishu iko hivi; Makambo amesajiliwa na Yanga msimu huu na hesabu za klabu hiyo ni kutaka jamaa acheze mechi zilizobaki za Kombe la Shirikisho Afrika, za hatua ya makundi.

MSHAMBULIAJI, Heritier Makambo, anaendelea kufunga mabao makali akiwa mazoezini Yanga, lakini kule Cairo, Misri mambo yamekuwa tofauti baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuizuia jezi yake atakayoitumia na kuirudisha nchini.

Usishtuke, ishu iko hivi; Makambo amesajiliwa na Yanga msimu huu na hesabu za klabu hiyo ni kutaka jamaa acheze mechi zilizobaki za Kombe la Shirikisho Afrika, za hatua ya makundi.

Tayari klabu yake ya zamani ya FC Lumpompo ilishamalizana na Yanga kwa kuituma hati yake ya uhamisho wa kimataifa (ITC), lakini jina lake na jezi atakayoitumia vilipowasilishwa CAF, wakubwa wakaigomea.

Yanga inataka Makambo atumie jezi namba 11 iliyotangaza ataivaa ambayo hapo kabla ilikuwa ikitumiwa na Mzimbabwe Donald Ngoma aliyetemwa na kutimkia Azam FC.

Lakini CAF imegoma kuipitisha jezi hiyo kwani Ngoma bado anasomeka ni mchezaji wa Yanga kama ilivyo kwa Obrey Chirwa licha ya kwamba washambuliaji hao wameshandoka Jangwani. Shirikisho hilo limewaambia Yanga kuwa mambo mengine yote kuhusu mshambuliaji huyo yapo sawa, lakini watafute jezi nyingine ambayo haijavaliwa na yeyote ndiyo itumiwe na mshambuliaji huyo.

Tayari Mwanaspoti linafahamu ofisi ya Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omari Kaya, imeshalifanyia kazi hilo kwa kutuma jezi nyingine ambapo sasa anaweza kutumia jezi namba tisa.

Jezi hiyo awali ilikuwa ikitumiwa na beki Mtogo, Vincent Bossou na msimu uliopita haikutumiwa na yeyote.

Hata hivyo, uwezekano wa Yanga kumtumia Makambo katika mchezo ujao dhidi ya USM Alger unategemea huruma ya CAF kutokana na muda wa kuwasilisha jina lake likiwa limekamilishiwa kila kitu kuwa umeshapita.

Uhakika wa Yanga kumtumia Makambo sasa ni katika mchezo wa mwisho dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda utakaopigwa Kigali.

Yanga ni kama imeshalainishiwa mambo kuelekea mchezo huo baada ya CAF kuwafungia wachezaji watatu muhimu wa Wanyarwanda hao kufuatia vurugu za mchezo wao dhidi ya USM Alger.

Caf limewafungia kiungo mkabaji Yannick Mukunzi, Chris Mbondi na kipa mkongwe, Kassim Ndayisenga, waliobainika kufanya vurugu katika mchezo ulioisha kwa sare ya bao 1-1.