Majimaji yaanza kujiwinda na Ligi Kuu

Muktasari:

Kocha msaidizi wa Majimaji, Habib Kondo alisema kuwa kupitia kambi hiyo, benchi la ufundi ndio litatoa hatma ya nyota watakaosajiliwa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Dar es Salaam. Baada ya ukimya wa muda mrefu, Majimaji FC inatarajia kuanza rasmi kambi yake ya maandalizi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu utakaonza Agosti 26.

Kocha msaidizi wa Majimaji, Habib Kondo alisema kuwa kupitia kambi hiyo, benchi la ufundi ndio litatoa hatma ya nyota watakaosajiliwa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

"Ni kweli tumechelewa kuanza kambi kwa sababu kuna masuala ambayo uongozi ulikuwa bado haujayakamilisha lakini kwa sasa kila kitu kipo sawa na tunatarajia rasmi kuingia kambini Ijumaa (kesho) tayari kwa kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao.

"Unajua sisi kama benchi la ufundi jukumu letu ni kuandaa ripoti na kuikabidhi kwa  viongozi ambao ndio wanaoshughulikia masuala ya kiutawala. Naamini tuna muda  wa kutosha kuiandaa timu na mashabiki wetu wasiwe na wasiwasi," alisema Kondo.

Kuhusu usajili, Kondo alisema kuwa wamechelewa kuanza kutokana na vurugu za timu kubwa ambazo zimekuwa zikitumia fedha nyingi kusajili.

"Sisi Majimaji ni timu ndogo hivyo hatuwezi kushindana na hao wenzetu katika vita ya usajili. Tumewaachia kwanza hao wenzetu watangulie kufanya vurugu zao, halafu  wakishamaliza nasi tutafanya usajili wetu," alisema kocha huyo.