Majeraha yamkosesha mwanariadha Ngorongoro Marathon

Arusha. Kocha wa riadha, Gidamis Shahanga amesema mwanariadha Kalisti Nade hataweza kurudi uwanjani mwaka huu kama alivyotarajia kutokana na kutopona vizuri mguu wake.

Mwanariadha huyo alipata ajali ya kugongwa na pikipiki mapema mwaka jana akiwa mazoezini huko Manyara na kusababisha kuvunjika mguu na meno kung’oka na kufanyiwa upasuaji na kufungwa vyuma vinne.

“Japo ameanza mazoezi mepesi, lakini sitaweza kumruhusu kwenda katika mashindano ya kwa kuwa itaweza kusababisha matatizo makubwa kwake japo nipo naye kwa karibu ili kuhakikisha anafuata maelekezo yangu pamoja na yale ya daktari,” alisema Shahanga.

Mwanariadha huyo alipatwa na mkasa huo wakati akijiandaa na mashindano ya kupata nafasi ya kuwa mmoja wa wakilishi wa timu ya Taifa iliyokwenda Uganda kwenye mashindano ya Nyika ya Dunia yaliyofanyika Machi 27 mwaka uliopita.

Nade yupo chini ya kituo cha michezo cha riadha “Shahanga Sports Institute” kinachomilikiwa na mwanariadha mkongwe Gidamis Shahanga huko Katesh ambaye alisema kuwa baada ya miaka kadhaa kituo hicho kitakuwa chimbuko la wanariadha.

“Sehemu ambazo aliathirika zaidi ni enka na sehemu za misuli na kusababisha afungwe chuma nne kubwa vikiwa miguu na chuma tatu ndogondogo zote zikiwekwa kwaajili ya kuunyosha mguu.”

Nade alisema kuwa alipenda kushiriki mashindano ya Ngorongoro yatakayofanyika Aprili 21 ikiwa ni moja ya kujiweka fiti lakini kocha wake hayupo tayari kumwona anajitumbukiza katika mashindano kwa madai ni hatari kwake.