Majaliwa ataka Umisseta kuibua Samatta wapya

Muktasari:

  • Akizungumza leo kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza wakati wa uzinduzi rasmi wa Michezo hiyo, Majaliwa amesema michezo hiyo ni fursa kwa wanafunzi kuonyesha vipaji vyao ili kuwafikia nyota Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaowakilisha nchi vyema katika soka kimataifa.

Mwanza. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wanafunzi wanaoshiriki michezo ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari nchini (UMISSETA)  na ile ya Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kutumia fursa hiyo ili kuwafikia kiwango cha wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Akizungumza leo kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza wakati wa uzinduzi rasmi wa Michezo hiyo, Majaliwa amesema michezo hiyo ni fursa kwa wanafunzi kuonyesha vipaji vyao ili kuwafikia nyota Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaowakilisha nchi vyema katika soka kimataifa.

Amesema kuwa michezo ni furaha, ajira na kuimarisha afya, pia ni husaidia kuleta matokeo mazuri kitaaluma.

Waziri huyo ameongeza kuwa michezo hiyo ni fursa kwa wanafunzi, hivyo mkoa ambao utamtumia mchezaji 'mamluki' Serikali itawachukulia hatua kali haswa kwa Maofisa Elimu Mkoa husika.

"Michezo hii ni fursa kwa wanafunzi tu na iwapo tutagundua kuwapo kwa 'Mamluki' kwenye mkoa wowote, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Maofisa Elimu" amesema Majaliwa.

Ameeleza Serikali imetoa fursa hiyo ikiwa ni mpango wa kuhakikisha nchi inapata timu za vijana imara ambazo zitalitangaza Taifa katika michezo kimataifa.

Kuhusu kiwango cha Michezo nchini

Waziri huyo ameongeza kuwa kwa sasa kiwango cha michezo kitaifa hakiridhishi na kwamba lazima pawepo mpango madhubuti.

Amesema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa Michezo lazima kuwepo msingi imara kuanzia chini.

"Pamoja na matokeo ya michezo kitaifa, bado kiwango hakiridhishi, lazima kuwepo msingi imara kuanzia ngazi za chini ikiwa ni kuweka mazingira mazuri ya miundombinu ikiwamo viwanja na wataalamu kwenye michezo," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Amewataka walimu wa michezo shuleni kuendeleza vipindi vya michezo kwa wanafunzi kwa kuwafundisha kivitendo na kinadharia.

"Niviombe Vyuo vya michezo nchini pia kuendelea kuzalisha wataalamu kwenye michezo ,lakini Halmashauri tengeni pesa kwa ajili ya kuendeshea michezo" amesema Majaliwa.