Magoli yenyewe ya ajabu ajabuuuu

Muktasari:

  • Bao la dakika ya 16 lililofungwa na kwa kichwa na Shiza Kichuya akiunganisha krosi ya Erasto Nyoni na hata lile la pili lililowekwa kimiani kipindi cha pili na James Kotei, yote yalikuwa gumzo kutokana na namna kipa wa Mbao alivyoyaruhusu.

SIMBA jana Alhamisi ilishindwa kukwea kileleni mwa Ligi Kuu Bara baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Mbao FC, lakini gumzo kubwa likiwa ni aina ya mabao yote manne yaliyofungwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa katika pambano hilo kali.

Bao la dakika ya 16 lililofungwa na kwa kichwa na Shiza Kichuya akiunganisha krosi ya Erasto Nyoni na hata lile la pili lililowekwa kimiani kipindi cha pili na James Kotei, yote yalikuwa gumzo kutokana na namna kipa wa Mbao alivyoyaruhusu.

Kichuya aliyeshindwa kumaliza kipindi cha kwanza baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna Niyonzima, aliruhusiwa kuruka mbele ya mabeki warefu wa Mbao na kumtungua kipa Kelvin Igendelezi.

Sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Habib Kayombo aliifungia Mbao bao la kusawazisha ambalo liliwaacha watu midomo wazi baada ya kuwa wa pili kuugusa mpira tangu ulipoanzishwa na Aishi Manula kukubali kutunguliwa.

Hilo lilikuwa bao la tatu kwa chipukizi huyo ambaye msimu uliopita aliwaliza Yanga kwenye uwanja huo katika mechi ya Ligi Kuu.

Dakika chache baadaye Kotei aliyecheza vema akishirikiana na Mzamiru Yassin, aliiandikia Simba bao la pili baada ya mabeki wa Mbao kufanya uzembe, lakini mtokea benchi Emmanuel Mvuyekule alisawazisha mambo baada ya kupiga shuti nje ya 18 katika dakika ya 81 na kumuacha kipa Manula akiwa hana la kufanya.

Sare hiyo imeifanya Simba kubaki nafasi ya pili ikiwa na pointi nane baada ya kucheza mechi nne na kushindwa kuiengua Mtibwa Sugar itakayocheza Pwani keshokutwa dhidi ya Ruvu Shooting. Mtibwa ipo kileleni kwa alama tisa baada ya mechi tatu.

Mbali ya kushindwa kukwea kileleni, lakini pia sare hiyo imeitibulia Simba ambayo ilikuwa haijaruhusu bao lolote katika mechi tatu za awali, pia imemtibulia kipa wao Aishi Manula aliyekuwa hajafungwa bao lolote.

Katika mchezo huo uliokuwa mkali, Mbao ilishuka uwanjani hapo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi tatu za msimu uliopita mbele ya Simba, zikiwamo mbili za Ligi Kuu na moja ya fainali ya Kombe la FA, hivyo ilicheza kwa tahadhari ikiwabana nyota wa Simba hasa Emmanuel Okwi na John Bocco.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Simba ugenini na wiki ijayo itaivaa Stand United mjini Shinyanga.

SIMBA:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Method Mwanjani, James Kotei, Shiza Kichuya/Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, John Bocco, Emmanuel Okwi, Nicholas Gyan/ Laudit Mavugo.