Mabosi wa Jangwani wapewa dili

Muktasari:

  • Jamaa wanafanya mambo yao kimya kimya. Hata hivyo, wanachama wameamua kuibuka na kuwapa mchongo wakiitaka Kamati ya Usajili kufanya usajili matata na wenye akili kwa kuwanasa mastaa wenye uzalendo na wanaojituma uwanjani.

KAMA unadhani viongozi wa Yanga wamelala katika suala zima la usajili basi utakuwa unajidanganya aisee.

Jamaa wanafanya mambo yao kimya kimya. Hata hivyo, wanachama wameamua kuibuka na kuwapa mchongo wakiitaka Kamati ya Usajili kufanya usajili matata na wenye akili kwa kuwanasa mastaa wenye uzalendo na wanaojituma uwanjani.

Mchongo huo umetolewa na shabiki kindakindaki wa Yanga, Athumani Kihamia, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, akisema kikubwa ni kufanya usajili wenye utulivu kwa kuwaleta kikosi wachezaji wenye uzalendo na kujituma.

Hata hivyo, amesema kuwa msimu uliopita Yanga ilishindwa kutamba kutokana na matatizo ya kiuchumi, lakini kikosi kilikuwa na wachezaji wa maana tu.

“Kuna wachezaji wana majina makubwa kwa kutajwa tu katika magazeti, lakini uwezo wao ulikuwa wa kawaida. Hawakuwa na maajabu na tulipoanza kuyumba kiuchumi ndio wakawa wa kwanza kuanzisha mgomo baridi na kutuletea matokeo mabaya,” alisema Kihamia.

Kutokana na hilo, ameishauri kamati ya usajili kuacha kusikiliza kelele za wachezaji wanaotajwa sana bali iangalie uwezo na uzalendo wa mchezaji husika. Naye Ernest Manyilizu aliiomba kamati hiyo kufanya usajili katika eneo la ulinzi na kiungo ambako ndio kunaonekana kuwa na shida.

Katibu wa Yanga Tawi la Arusha, Destrich Kateule, alisema watajitoa kuchangia ili kuondokana na kikwazo cha kiuchumi ndani ya klabu yao.