Mabosi TFF wawakingia kifua Kili Stars

SHIRIKISHO la Soka la Tanzania (TFF), limefafanua juu ya wachezaji wa Kilimanjaro Stars ambao walionekana kuvalia  vipensi badala ya kuwa kwenye mavazi maalumu ya Taifa kikosi hicho kilipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limezua sintofahamu kwa wadau wengi ambao wamehoji juu ya waliokuwa wakikisimamia kikosi hicho ambacho kilibeba dhamana ya kuiwakilisha Tanzania Bara.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alifafanua jambo hilo kwamba waliwapokea wachezaji saa 2:30 asubuhi juzi  Jumanne wakitokea Kenya kwenye Kombe la Chalenji wakiwa wamevaa sare maalumu za timu.

“Lakini baada ya kuwasili, baadhi ya wachezaji walisema hawaoni haja ya kwenda hotelini, badala yake walivua zile sare na kuvaa mavazi wanayoona yanawafaa wakati wakienda majumbani mwao,” alisema.

“Lakini walifika wakiwa kwenye sare kwani hilo ni jambo tunalolisisitiza, hivyo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii ufafanuzi wake ndio huo.”

Aidha Lucas alisema michuano ya Kombe la FA itaendelea Desemba 20 na kwamba katika hatua ya sasa,  timu mwenyeji itakuwa inapewa Sh1.5 milioni huku timu inayosafiri ikipewa mara mbili yake.

“Pesa hizo zilitalipwa kupitia akaunti ya klabu na si kiongozi, ambao hawajaleta akaunti zao wawahishe ili waweze kufanya maandalizi yao mapema, hatutampa mtu pesa mkononi,” alisema.