Mabingwa wa Mkoa wa kati Kombe la Wanyama wajulikana!

Nairobi. BAADA ya mikoa sita kupata wawakilishi wa fainali za kitaifa za michuano ya Chapa Dimba, hatimaye mabingwa wa mkoa wa kati kwa akina dada na wavulana wamepatikana leo.
Mabingwa hao ambao  watauwakilisha mkoa huo walipatikana katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye uga wa Chuo cha ufundi cha Thika.
Bingwa kwa upande wa akina dada ni Limuru Starlets ya Limuru huku Euro Nuts wakitawazwa mabingwa kwa upande wa wavulana.
Limuru Starlets waliibuka mabingwa kwa kuitandika Rwambiti ya Kirinyaga mabao 6-0 katika mchezo mkali wa fainali uliopigwa kuanzia saa tatu asubuhi.
Wakicheza kwa kiwango cha juu tangu mwanzo, Limuru Starlets waliwaduwaza Rwambiti kwa kujipatia mabao matatu ya haraka yaliyofungwa na Faith Atieno (10), Millicent Njoki (21) na Latonia Atieno (34).
Kipindi cha pili cha mchezo huo ulianza kwa kasi ya kawaida huku malkia wa Limuru wakiamua kubadili mfumo kutoka 4:4:2 kwenda 5:3:2 kwa lengo la kujilinda zaidi mbinu ambayo ilifanikiwa kwa kiasi fulani.
Katika dakika ya 49, Rwambiti walicharuka na kuliandama lango la wapinzani wao ikiwa ni harakati za kurekebisha makosa ya kipindi cha kwanza yaliyopelekea kubugizwa mabao ya haraka.
Kuona wanashambuliwa sana, kocha wa Limuru Queens, James Kaivu, alibadili mfumo kwa kujaza viungo (3:5:2) huku akiwatumia mawinga wake Atieno Latonia na Wanjiru Alice.
Mbinu hii iliwachanganya zaidi Rwambiti na kujikuta wakipotezana kitendo kilichompa mwanya mshambuliaji hatari, Millicent Njoki, kugongelea misumari mitatu 'hat trik' katika sanduku la Rwambiti kunako dakika ya 60, 75 na 87.
Kwa upande wa wavulana, Euro Nuts walitawazwa mabingwa wa mkoa wa kati baada ya kuwalaza wapinzani wao wa jadi, Lufa Boys kutoka Laikipia kwa goli 1-0, lililopachikwa wavuni na Lauren Emmanuel katika dakika ya 12.
Kwa ushindi huo, Euro Nuts na Limuru Queens wamejishindia kitita cha Ksh. 200, 000, Kombe, Simu na muda wa maongezi kila mmoja na fursa ya kuwakilisha mkoa wa kati kwenye fainali.
Mfungaji bora kwa wanawake ni Millicent Njoki aliyefunga mabao matano, Kipa bora ni Susan Njeri (wote kutoka Limuru Queens), huku mchezaji bora akiwa ni Veronica Wairimu wa Good girls ya Thika.
Kwa upande wa wanaume, mfungaji bora ikienda kwa wachezaji watano ambao walikuwa na goli moja kila mmoja, kipa bora ni David Wainaina (Euro Nuts) na mchezaji bora akiwa ni John Njuguna (Euro Nuts). Zawadi kwa mfungaji bora, kipa bora na  mchezaji bora ni Ksh. 30,000.
Mpaka sasa jumla ya mikoa saba ambayo ni Kati, Rift Valley, Eastern, Nyanza, North Eastern, Coast na Western imeshapata wawakilishi watakaoshiriki fainali ya Kitaifa, huku mkoa wa Nairobi ukisubiriwa kupata wawakilishi.
Fainali za kitaifa za michuano hiyo ya Chapa Dimba, inashirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 15-20 na kudhaminiwa na kampuni ya simu ya Safaricom, zitafanyika machi 24-25, kwenye dimba la Bukhungu, Mjini Kakamega na kushuhudiwa na balozi wake.
Balozi wa michuano hiyo ni Kiungo wa Tottenham Hotspurs na Nahodha wa Harambee Stars, Victor Mugubi Wanyama.