Mabeki wa kati wenye pesa ndefu duniani

Muktasari:

Kawaida kwenye soka, washambuliaji na viungo ndiyo wachezaji wanaopewa nafasi kubwa za kulipwa pesa nyingi na kuwa matajiri tofauti na mabeki na makipa.

LONDON, ENGLAND. UMESHAMWONA Chiellini anatetemeka anapomkaba Cristiano Ronaldo? Hawezi kufanya hivyo kwa sababu anafahamu wazi kabisa anacheza na tajiri mwenzake.

Kawaida kwenye soka, washambuliaji na viungo ndiyo wachezaji wanaopewa nafasi kubwa za kulipwa pesa nyingi na kuwa matajiri tofauti na mabeki na makipa. Kuna wachezaji kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Neymar, Alexis Sanchez, Mesut Ozil na hata Paul Pogba, wanalipwa vizuri kweli kweli na ndio maana NI matajiri.

Lakini, kuna mabeki pia viwango vyao matata vimewafanya walipwe pesa ndefu na hivi unavyosoma makala haya ni matajiri wakubwa duniani.

Hii hapa orodha ya mabeki watano wenye pesa ndefu ambao, bado wapo uwanjani kwa sasa kupambana na washambuliaji wakorofi kama Luis Suarez, Zlatan Ibrahimovic, Diego Costa na wengineo. Mabeki wa kati matajiri wanaocheza kwa sasa duniani.

5. Giorgio Chiellini- Juventus

Utajiri: Dola 43 milioni

Beki huyo Mtaliano amekuwa mtu muhimu kweli kwenye Serie A akiwa na kikosi cha Juventus. Kiwango chake bora kimeleta mkwanja mrefu na hivyo kuwa, miongoni mwa mabeki wenye pesa ndefu duniani. Usimwone Chiellini anakaza vile ndani ya uwanja kiasi cha kumfanya hata afikie kung’atwa na Luis Suarez, anafahamu huduma hiyo ndiyo inayoleta maisha mazuri nyumbani. Kipato chake ni Dola 43 milioni.

4. Vincent Kompany- Man City

Utajiri: Dola 45 mil

Beki wa Kibelgiji, Vincent Kompany ameanza kurudi kwenye ubora baada ya kuwa na misimu kadhaa mibaya. Shida yake kubwa ni majeruhi ya mara kwa mara huku umri nao ukiwa kikwazo kingine na haonekani kama tatizo hilo linaondoka kabisa kwa kipindi cha karibuni. Lakini, hilo halijawahi kuwa shida katika kumfanya asipige pesa na hata akiamua kustaafu sasa, Kompany ana kipato kinachofikia Dola 45 milioni.

3. Thiago Silva- PSG

Utajiri: Dola 46 milioni

PSG ililipa pesa ndefu kupata huduma ya Thiago Silva na Zlatan Ibrahimovic ilipowanasa kutoka AC Milan miaka kadhaa iliyopita na hakika huo ulikuwa uwekezaji mkubwa katika kikosi hicho cha Paris, Ufaransa. Baada ya miaka mitatu yenye mafanikio makubwa, Ibrahimovic ameondoka, lakini Mbrazili Silva bado yupo kwenye kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na Unai Emery. Huduma bora ndani ya uwanja imemfanya Silva kuvuna pesa za kutosha na hivyo, kumfanya awe na kipato cha Dola 46 milioni.

2. Gerard Pique- Barcelona

Utajiri: Dola 58 milioni

Gerrard Pique hakuwa akifahamika sana wakati alipoisaidia Manchester United kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008 katika fainali ambayo walicheza na Chelsea huko Moscow, Russia. Lakini, aliporejea kwenye timu yake ya zamani ya Barcelona, huko alikwenda kutangaza jina lake na kuliweka kwenye viwango vya juu kabisa kwenye soka la dunia. Amedumu kwenye soka la kiwango cha juu kwa muda mrefu na kuvuna pesa za kutosha zinazomfanya awe na jeuri ya kumiliki penzi la mrembo matata wa Colombia, Shakira. Pique ana kipato cha Dola 58 milioni.

1. Sergio Ramos-Real Madrid

Utajiri: Dola 60 milioni

Nahodha wa Real Madrid, beki wa kati Sergio Ramos ni mfano halisi wa kiongozi kwenye timu. Mara nyingi tu amekuwa akijipa majukumu ya kuhakikisha timu inapata matokeo bora ndani ya uwanja kwa kupanda mbele kwenda kuwasaidia washambuliaji kufunga mabao. Hakuna asiyefahamu namna Ramos anavyoibeba timu hiyo mfano rahisi ni ile fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2013, na Atletico Madrid ilibaki sekunde chache tu watwae ubingwa, lakini Ramos alipindua matokeo hayo na kuisaidia Real Madrid kushinda. Ramos ni beki tajiri na kipato chake kinatajwa kuwa ni Dola 60 milioni.