Mabao yao yazipaisha Simba, Yanga, Azam

Muktasari:

  • Mabao ya washambuliaji hao yamechangia pointi nyingi kwa klabu hizo

Namba hazidanganyi... Bila ya mabao ya Shiza Kichuya, Mbaraka Yusuf na Ibrahimu Ajib

vinara wa Ligi Kuu Simba, Azam na Yanga zingekuwa katika hali mbaya.

Simba inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 22 sawa na Azam inayoshika nafasi ya pili huku Yanga ikiwa nafasi tatu na pointi 20 baada ya kuchezwa kwa mechi 10.

Pamoja na Emmanuel Okwi, Obrey Chirwa kuongoza katika chati ya  ufungaji bado mabao yao hayana

thamani kuzidi  yale yaliyofungwa na Watanzania hao.

Okwi wa Simba ndio anaongoza akiwa amefunga mabao manane akifutiwa na Obrey Chirwa wa Yanga

aliyefunga mabao sita.

Mtandao wa Mwanaspoti limeangalia mchango wa washambuliaji hao watatu Kichuya, Yusuf na Ajib

katika timu zao na kubaini kuwa kama wasingefunga basi timu hizo zingekuwa katika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi.

Ibrahim Ajib aliyesajiliwa na Yanga msimu huu ameonekana kuwa na msaada mkubwa zaidi kwa timu hiyo kwani amechangia pointi 12 mpaka sasa.

Kama Ajib asingechangia pointi hizo basi Yanga hivi sasa ingekuwa nafasi ya 13 au 14 kwenye msimamo wa ligi kwani ingekuwa na pointi nane tu.

Ajib mwenye mabao matano kwenye ligi, aliamua matokeo ya ushindi wa Yanga katika mchezo dhidi ya Njombe Mji ambayo Yanga ilishinda bao 1-0 na mfungaji akiwa yeye,huku pia akifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Ndanda ambao Yanga ilishinda bao 1-0.

Pia, mchezaji huyo wa zamani wa Simba  alichangia ushindi wa mabao 2-1 ilioupata timu yake ugenini dhidi ya Kagera Sugar baada ya kufunga bao la pili na la ushindi. Katika mchezo huo Chirwa alianza kuifungia timu yake bao moja na kama  Ajib asingefunga katika mchezo huo basi matokeo yangekuwa sare ya 1-1 hivyo Yanga ingeambulia pointi moja tu.

Ajib pia alichangia kwa kiasi kikubwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 ugenini dhidi ya Stand United baada ya kuifungia timu yake mabao mawili huku mengine yakifungwa na  Pius Buswitea na Chirwa. Hivyo hata kama Buswita na Chirwa wasingefunga siku hiyo Yanga bado ingeshinda kupitia Ajib pekee aliyefunga mabao mawili ya mapema.

 

Kwa upande wa Simba,licha ya jina la Okwi kuchomoza sana na kuonekana ndio nyota wa timu hiyo lakini Shiza Kichuya ameonekana kuibeba timu hiyo zaidi kwa mabao yake yaliyoamua matokeo na pasi nyingi za mabao.

Okwi amefunga  katika mechi tatu lakini akifunga mabao mengi katika mechi mbili ambazo pia hata kama asingefunga mabao hayo bado Simba ingeshinda kupitia mabao ya wengine lakini anapata pointi moja baada ya kuibeba timu yake katika mchezo mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 90 ya mchezo na kuwa sare ya 1-1 hivyo kuinusuru timu yake na kipigo.

Kichuya mwenye mabao matano kwenye ligi ameipa Simba pointi saba kati ya 22 ilizonazo hivyo kama asingechangia pointi hizo wekundu wa Msimbazi wangekuwa nafasi ya sita au saba kwenye msimamo wa ligi kwani wangekuwa na pointi 15.

 Kichuya amechangia kuipa pointi timu yake katika ushindi wa mabao 2-1 ambao Simba ilipata  dhidi ya Stand United na yeye akifunga bao la kwanza na lingine la ushindi likiwekwa kimiani na Laudit Mavugo.

Pia aliibeba timu yake katika mchezo dhidi ya Yanga ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 halafu akaipa pointi tatu muhimu Simba katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

Kwa Azam mshambulliaji Mbaraka Yusuph ndiye ameibeba timu hiyo zaidi akichangia pointi tisa kati ya 22 ambazo wanalambalamba hao wamekusanya hadi sasa na kama mchezaji asingechangia pointi hizo basi Azam ingekuwa nafasi ya  saba kwani ingekuwa na pointi 13.

Tangu kuanza kwa msimu huu Azam imeweka rekodi ya kushinda bao moja moja katika mechi zake huku Mbaraka akifunga mabao matatu kati manane ambayo yamefungwa  na timu hiyo hadi sasa kwenye ligi.

Mbaraka aliipa timu yake pointi tatu muhimu katika ushindi wa Azam wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Suagr pia aliifungia timu hiyo katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya  Lipuli.

Mshambuliaji huyo aliyeichezea Kagera Sugar msimu uliopita aliipa tena pointi tatu muhimu timu yake katika mchezo dhidi ya Mbeya City ambao Azam ilishinda bao 1-0.