Maandalizi mashindano Kanda ya Tano mambo ni moto!

Wednesday July 11 2018

 

By Brown Msyani

Dar es Salaam. Chama cha Mchezo wa Kikapu Tanzania [TBF],  imeanza kukarabati Uwanja wa Ndani wa Taifa utakaotumika kuchezewa  mashindano ya mpira wa kikapu ya Kanda ya Tano ya Afrika.

Mashindano hayo ya Kanda ya Tano ya Afrika yanatarajia kuanza Septemba mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Katika mashindano hayo timu za taifa zitakazoshiriki mashindano hayo ya kanda zitatoka   Misri, Uganda, Kenya, Rwanda, Sudani, Ethiopia, Burundi, Somalia na wenyeji Tanzania.

Mwananchi ilikuwepo uwanjani hapo jana  ilishuhudia kamisheni wa ufundi  wa TBF, Manase Zabron akianza kazi ya upakaji rangi uwanjani hapo.

Akiongea katika mahojiano mahalumu na mwandishi wa habari hizi jana , Zabron alisema TBF imepania kutofanya makosa kama walivyofanya ya kushindwa kukarabati Uwanja wa Ndani wa Taifa wakati wa  mashindano ya umri wa chini ya miaka 18.

“Kweli ilikuwa ni aibu katika mashindano hayo ambapo tulishindwa kupaka rangi uwanja,kurekebisha viti,vyoo na magoli ya kuchezea,” alisema Zabron.

Kwa mjibu wa kamisheni huyo mipango waliyopanga ni kurekebisha vyoo pamoja na maeneo yatakayotumika kukaa watazamaji mapema kabla ya mashindano hayo kuanza.

Naye Katibu Mkuu wa TBF Michael Mwita alisema licha ya Serikali kuhaidi kukarabati uwanja  bado wanaangaika kutafuta wafadhiri watakaorekebisha miondomindu ya ndani ya uwanja.

“Mwaka huu  tumepania kufanya maajabu  ya kuwa na uwanja mzuri pamoja na timu zetu za taifa kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa ya Kanda ya Tano ya Afrika," alisema Mwita.

Hata hivyo wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika ya vijana wa umri wa miaka 18, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema  Serikali itafanya kila linalowezekana kufanya marekebisho makubwa ya uwanja huo.