Maajabu ya Cristiano Ronaldo

SUPASTAA wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amerudi kwenye ubora wake. Staa huyo wa kimataifa wa Ureno anatupia tu.

Watu walimwona kachoka mwanzoni mwa msimu, lakini ghafla tu amebadili kibao na sasa amekuwa tishio kuliko neno tishio lenyewe. Mreno huyo amefunga mabao 21 katika mechi 13 alizocheza tangu mwaka huu wa 2018 uanze. Katika mechi za La Liga tu, mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Dunia amefunga 17 katika mechi nane tu. Ukitaka hesabu za jumla kwenye michuano yote amefunga mabao 37.

Kwa rekodi hizo za Ronaldo za kupasia mipira nyavuni tangu mwaka huu uanze, amezifunika klabu kibao vigogo kwenye Ligi Kuu Tano Bora za Ulaya, ambazo hazimuwezi Mreno huyo kwa mabao yao waliyofunga kwenye ligi.

5. Chelsea- mabao 14

Kocha wa Chelsea, Antonio Conte, hatafurahishwa kabisa na washambuliaji wake kama ataziona takwimu hizi za mabao ya Ronaldo. Wakati staa huyo katupia mara 21 katika mechi 13 tangu Januari, 17 yakiwa ya La Liga pekee, Chelsea ina mabao 14 kwa muda huo. Hiyo inaonyesha ubutu wa fowadi ya wababe hao wa Stamford Bridge, ambao tangu Januari 13, mastraika wake Alvaro Morata na Olivier Giroud kila mmoja amefunga bao moja. Itawakumbuka Michy Batshuayi na Diego Costa.

4. B/Dortmund- mabao 15

Michy Butshuayi tangu atue Borussia Dortmund kwa mkopo katika dirisha la Januari amefunga mabao manane akicheza kwa mkopo kutoka Chelsea. Lakini, mchango wa wachezaji wengine kwenye kufunga mabao si mzuri kabisa, jambo linalowafanya wabeba hao wa Bundesliga kufunga mabao 15 tu tangu mwaka huu uanze na kuzidiwe na Ronaldo kwa mabao mawili kwa yale ya ligi tu bila ya kuhesabia aliyofunga katika michuano mingine.

3. Arsenal- mabao 17

Arsenal imekuwa ikitaabika kwa miezi ya karibuni. Sababu inaonekana wazi kabisa, haifungi mabao ya kutosha. Kumbukumbu pekee wanayokumbuka kwenye mechi zao za mwaka huu ni ule ushindi wao wa mabao 5-1 dhidi ya Everton walipocheza huko Emirates. Wiki iliyopita walifunga mabao matatu dhidi ya Watford kuwafanya kufikisha idadi ya mabao 17, ikiwa ni sawa na mabao ya Ronaldo aliyofunga kwenye La Liga peke yake. Ukichanganya michuano yote, Mreno huyo ana mabao manne zaidi ya waliyofunga mastaa wa Arsenal wote akiwamo Pierre-Emerick Aubameyang, Alexandre Lacazette, Danny Welbeck na wengineo ukichanganya pamoja.

2. AC Milan- mabao 17

Ikijaribu kurejea kwenye makali yake, AC Milan ilijikuta ikigonga kisiki baada ya kutupwa nje ya michuano ya UEFA Europa League na wababe wa London, Arsenal wiki iliyopita. Shida yao kubwa AC Milan wanaonolewa na Gennaro Gattuso ipo kwenye kufunga mabao. Gattuso hapati huduma bora kutoka kwa mshambuliaji wake Andrian Silva na mbadala wake Fabio Borini naye hana maajabu. Ukichukua mabao aliyofunga kwa La Liga tu, Ronaldo amelingana na mabao yote waliyofunga AC Milan kwenye michuano yote waliyocheza tangu mwaka huu uanze.

1. Man United- mabao 17

Jose Mourinho amekuwa akitumia maneno mengi sana kujitetea kwa siku za karibuni hasa baada ya kikosi chake cha Manchester United chenye thamani kubwa kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Sevilla. Mashabiki na wachambuzi wa soka wanashindwa kabisa kuelewa inakuaje kwa timu kama Man United inateswa katika mechi zote mbili ilizocheza dhidi ya Sevilla na hatimaye kuondoshwa kwenye michuano hiyo. Presha ya Man United pia imekuwa kubwa kutokana na kasi ya wapinzani wake kwenye Ligi Kuu England, Manchester City na Liverpool, wanaonekana suala la kufunga mabao halijawahi kuwa tatizo kwa upande wao. Kuonyesha kwamba Man United ya Mourinho ina hali mbaya zaidi baada ya kugundua kwamba mabao yao yote waliyofunga yanalingana na aliyofunga Ronaldo kwenye La Liga tu tangu mwaka 2018 uanze. Straika Romelu Lukaku anafunga mabao, lakini tatizo ni washambuliaji wengine wanaomzunguka, kama vile Alexis Sanchez, Anthony Martial na Marcus Rashford hawana maajabu.