MSALA: Amunike shughuli yake ipo hapa tu

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) walimtangaza Mnigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha wa timu ya Taifa Stars ambayo inajiandaa kufuzu michuano ya AFCON na mwezi ujao watacheza dhidi ya Uganda.

Rais wa TFF, Wallece Karia alipomtangaza Amunike wiki moja iliyopita alisema atakuwa kocha mkuu wa Taifa Stars na timu za vijana chini ya umri wa miaka U-17, U-20 na U-23.

Amunike amechukua nafasi hiyo kutoka kwa mzawa, Salum Mayanga ambaye amekwenda Mtibwa Sugar kuwa Mkurugenzi wa Ufundi akishirikiana na benchi la ufundi lililo chini ya Zubery Katwila.

Mwanaspoti lilifanya tathimini fupi ya mambo matano ambayo Amunike anatakiwa kuanza nayo katika kikosi cha Taifa Stars kwa muda wa miaka miwili na atakuwa anafanya kazi kabla ya kuingia makubaliano mengine ya nyongeza kama mkataba wake unavyosema.

UTEUZI SAHIHI

Mara nyingi kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wadau wa soka nchini kuwa kikosi cha Taifa Stars ambacho kinaitwa kwa nyakati tofauti kinakuwa na mapungufu kwa kukosa baadhi ya wachezaji ambao wanafanya vizuri.

Vile vile kulikuwa na taarifa makocha wa Taifa Stars wanaingiliwa katika majukumu yao ya kuteua wachezaji ambao anawataka kulingana na mechi husuka na wanawaita kutokana na matakwa ya viongozi fulani.

Amunike kibarua cha kwanza ambacho natakiwa kuanza nacho ni kufuta malalamiko hayo kwa kufuatilia wachezaji katika ligi mbalimbali na kuchagua ambao wanafanya vizuri kwenye vikosi vyao.

Isiwe timu yenye kuonyesha uwepo wa kuiteua kwa kufuata majina bala kuangalia viwango.

MAENDELEO YA WACHEZAJI

Tanzania kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje ya mipaka ya nchi lakini wanashindwa kutambulika kutokana na ufuatiliaji mdogo ambao unafanyika dhidi yao.

Kama umekuwa msomaji mzuri wa Mwanaspoti toleo la Jumatatu (Nje ya Bongo) limekuwa likigusa baadhi ya wale wachezaji wengi ambao wanacheza soka Ulaya na Afrika lakini bado hakuna ufuatiliaji mkubwa na wa uhakika.

Wachezaji wengine wa Tanzania ambao wanacheza nje hujikuta wanabadili uraia wa nchi pengine ni kutokuwa na ukaribu, ufuatiliaji wa kutosha kutoka hapa nchini hasa wenye dhamana na mchezo husika ama benchi la ufundi.

Amunike atakuwa na kibarua cha kuwafuatilia wachezaji hawa wengi ambao wanacheza nje na kutafuta njia sahihi ya kuwakutanisha kwa pamoja au kuwafuaitilia kwa karibu huenda wakaongeza kitu Taifa Stars.

Nyota Mbwana Samatta, Saimon Msuva, Farid Mussa, Himid Mao, Abdi Banda, Shaban Chilunda ni baadhi ya wanaocheza nje na kufahamika hapa nchini lakini Amunike akifuatilia kwa ukaribu atawapata zaidi ya hao.

KUWAPA NAFASI VIJANA

Mataifa mengi ya Afrika yanafanikiwa zaidi katika soka kutokana na uwekezaji kwenye soka la vijana ndio maana kila kizazi ambacho kinaondoka kikiwa bora katika timu zao za Taifa wanaingia wengine na wanaendeleza.

Viongozi wa soka hapa Tanzania wamekuwa si wamafuatiliaji na kuwekeza kwa uhakika soka la vijana ambalo ndio msingi wa soka unapopatikana licha ya baadhi ya timu za vijana kufanya vizuri.

Amunike anarekodi nzuri katika soka la vijana na huenda akafanya vizuri kuwapa nafasi vijana timu ya Taifa Stars lakini hiyo nayo ni sehemu muhimu ambayo anatakiwa kuifanyia kazi ipasavyo.

USIMBA NA UYANGA

Ukiangalia mara nyingi kikosi cha Taifa Stars kila kinapoteuliwa kunakuwa na nyota wengi wa Simba na Yanga kwa wakati huo hutegemea timu ipi ambayo inafanya vizuri katika Ligi Kuu Bara na wachezaji wake watakuwa wengi kikosini.

Muda mwingine uteuzi huo umekuwa na malalamiko mengi lakini ukweli usiopingika timu hizo ndizo zinafuatiliwa zaidi katika kila mechi ambazo wanacheza kuliko timu nyingine yoyote hapa nchini.

Kama kocha Amunike atapata bajeti ya kutosha kuzunguka na kufuatilia ligi mbalimbali ambazo wachezaji kutoka Tanzania wanacheza ataona vipaji na wachezaji wengi ambao wanavigezo vya kucheza Taifa Stars.

Amunike anatakiwa kuondoa Usimba na Uyanga ndani ya kikosi cha Stars kwa kuzunguka kila kona ili kuona wachezaji wote lakini kama kuna wale ambao wanastahili kucheza kikosi hicho na wanatoka timu za Simba na Yanga wapewe nafasi.

MECHI NGUMU

Amunike atakuwa anafahamiana na mawakala au makocha wenzake wakubwa wengi jambo ambalo anatakiwa kutafuta mechi nyingi za kirafiki kila kalenda ya Fifa itakavyokuwa inaonyesha.

Mechi hizo hazitakiwi kuwa za kawaida bali ni zile timu ngumu na kubwa Afrika hata Ulaya kwani kama ikiweza kucheza na kupata matokeo mazuri dhidi ya timu hizo zitapatikana faida nyingi kama wachezaji kuonekana, kupanda viwango na nyingine nyingi.

Amunike kwa ukubwa wake ni wazi jukumu hili la kutafuta mechi nyingi na kubwa za Kimataifa litakuwa mikononi mwake kwa muda wote wa miaka miwili ambao atakuwa akizinoa timu zote za Taifa.