MPIRA PESA UNAAMBIWA

LONDON, ENGLAND. UNAAMBIWA hivi, mpira pesa. Ukitaka kufahamu hilo, tazama usajili wa wachezaji unavyofanyika duniani kwa sasa, wachezaji wote wazuri kuwapata ni lazima utumie pesa nyingi kweli kweli.

Huko Ulaya, pesa inamwagwa tu, si kwenye Ligi Kuu England, La Liga, Ligue 1 wala kwenye Serie A, mpira umehamia kwenye pesa na hiyo ndiyo inayoonekana kuwa njia sahihi ya kuwa mshindani kwenye soka la kisasa.

Makocha, mashabiki na wachambuzi wa soka wamekuwa wakilalamika kila siku kwamba siku hizo usajili wa wachezaji imekuwa biashara inayotia kichaa. Maisha ndivyo walivyokimbia kwa kasi kiasi hicho.

Lakini, unahitaji nini tena, ukiwa na pesa na kuwa na kikosi kama hiki, ubingwa gani utakupita na usiubebe? Hiki hapa Kikosi cha Kwanza ghali zaidi duniani kwa sasa, na wachezaji wote wamegharimu pesa ndefu, Pauni 1.09 bilioni.

Kipa- Pauni 71.6 milioni

Habari ndiyo hiyo, kuna kipa amesajiliwa kwa Pauni 71.6 milioni. Dunia kwa sasa imebadilika, Pauni 71.6 milioni ilikuwa pesa inanyoweza kusajili washambuliaji, lakini kwa sasa inatumika kumsajili kipa.

Chelsea walivunja rekodi ya dunia kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya wakati walipomnasa kipa Kepa Arrizabalaga kutoka Athletic Bilbao kwa uhamisho wa Pauni 71.6 milioni. Pesa hiyo pengine itakaa kwa muda mrefu sana isivunjwe kwa miaka ya karibuni, labda hadi hapo David De Gea atakapoamua kuachana na Manchester United. Hata hivyo, Kepa alikuwa kipa mwingine kusajiliwa kwa pesa nyingi kwenye dirisha hilo la majira ya kiangazi kwani mwanzoni tu, Liverpool, walilipa Pauni 67 milioni kumnasa kipa wa Kibrazili, Alisson Becker kutoka AS Roma.

Mabeki wa kati- Pauni 133.5 milioni

Ligi Kuu England ndiyo inayomiliki rekodi ya kuwa na mabeki wa kati ghali zaidi duniani kwa sasa. Jambo hilo limekuja baada ya Liverpool kuamua kulipa Pauni 75 milioni kunasa huduma ya beki wa Kidachi, Virgil van Dijk kutoka Southampton kwenye dirisha la usajili lililofanyika Januari mwaka huu.

Wakati kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp akivunja rekodi hiyo ya dunia kwa kunasa beki kwa pesa nyingi, mwenzake Pep Guardiola wa Manchester City naye alifanya usajili mkubwa kweli kweli kwenye dirisha hilo hilo la Januari wakati alipomnasa Aymeric Laporte kwa Pauni 58.8 milioni. Mabeki hao wawili wa kati wa Liverpool na Liverpool ndio walionaswa kwa pesa nyingi zaidi duniani kwa sasa na rekodi yao ingevunjwa kama Manchester United wangefanikiwa kwenye usajili wao wa kumnasa Raphael Varane wa Real Madrid, ambapo iliripotiwa Man United ilikuwa tayari kulipa Pauni 100 milioni.

Mabeki wa pembeni- Pauni 99.25 milioni

Manchester City ndiyo timu inayomiliki rekodi ya kusajili mabeki wa pembeni kwa pesa nyingi duniani. Wababe hao wa Etihad, ambao ndio mabingwa watetezi kwenye Ligi Kuu England walilipa Pauni 51.75 milioni na Pauni 47.5 milioni kumnasa beki wa kushoto Benjamin Mendy na beki wa kulia Kyle Walker kutoka AS Monaco na Tottenham Hotspur kama walivyopangwa.

Mabeki hao wa pembeni ndio ghali zaidi duniani kwa sasa. Uwekezaji huo ulilipa kwa kocha Pep Guardiola kwani walikiwezesha kikosi cha Man City kubeba mataji mawili msimu uliopita, Ligi Kuu England na Kombe la Ligi. Thamani yao kubwa inawafanya mabeki hao wa pembeni kuingia kwenye kikosi hiki cha wachezaji ghali duniani.

Viungo- Pauni 361.3 milioni

Philippe Coutinho ndiye kiungo ghali zaidi duniani kwa sasa. Wakati anang’oka Liverpool kwenda Barcelona kwenye dirisha la Januari wababe hao wa Nou Camp walilipa kiasi cha Pauni 142 milioni kupata huduma yake. Pesa iliyolipwa awali ni Pauni 105 milioni, lakini kwa kuongeza nyongeza nyingine zinafanya mkwanja huo kufikia Pauni 142 milioni.

Barcelona baada ya kushtuliwa na kuondoka kwa Neymar wakaingia sokoni haraka sana kusaka mpara wake ndipo hapo ilipokwenda kutumia Pauni 130 milioni kunasa huduma ya staa wa Borussia Dortmund, Ousmane Dembele. Safu hiyo ya viungo ghali inakamilishwa na supastaa wa Manchester United, Paul Pogba, ambapo Mfaransa huyo alirudi Old Trafford akitokea Juventus kwa pesa nyingi baada ya kuigharimu klabu yake hiyo ya zamani Pauni 89.3 milioni ilipomsajili tena.

Washambuliaji- Pauni 425.8 milioni

Kwenye kikosi hiki, safu ya ushambuliaji inaundwa na wakali watatu matata kweli kweli, wakikosa ukachinje kuku. Cheki wakali waliopo kwenye fowadi ya kikosi hiki ghali kabisa duniani, ni masupastaa Neymar, Cristiano Ronaldo na Kylian Mbappe.

Neymar alitua PSG kwa ada ya Pauni 199.8 milioni akitokea Barcelona mwaka jana. Wababe hao wa Ufaransa, walikamilisha usajili mwingine wa pesa nyingi, ilipolipa Pauni 121 milioni kunasa saini ya Kylian Mbappe kutoka AS Monaco. CR7 aliwaduwaza mashabiki wengi wa soka alipoamua kuachana na Real Madrid na kwenda kujiunga na Juventus kwa dili linalodaiwa kuwa la Pauni 105 milioni. Kuwa na washambuliaji hao watatu wanafanya kikosi hicho kuwa na thamani ya Pauni 1.09 bilioni.