Lwandamina akenua ratiba Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

Mzambia huyo anarekodi ya kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa ya klabu barani Afrika

 KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina amefurahishwa na ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupawa dhidi ya timu ya Shelisheli.

Lwandamina amewapa mchongo mabosi wake kuwa klabu nyingi kubwa za Afrika huwa zinajipanga mapema kupata matokeo bora katika mashindano mbalimbali yanayosimamiwa na CAF, jambo ambalo na wao walifanye sasa.

 Lwandamina alisema klabu nyingi kubwa za Afrika zimekuwa zikiwapa motisha kubwa wachezaji wao kwa kuwaandalia viwango vya maana vya posho katika mechi hizo.

Lwandamina alisema ni vema mabosi wa Yanga nao wakaangalia mpango huo kwa kuwatia hamasa wachezaji kwa kuwaongezea mzigo wachezaji ili kujitoa uwanjani kuipelekea timu yao mbali katika michuano hiyo ya Afrika.

"Timu nyingi zinazofanya vizuri katika mashindano hayo hilo halitokei kwa bahati mbaya au kupendelewa wanajua kujipanga vyema na hatua ya kwanza ni kutengeneza timu na kuwatengeneza wachezaji kisaikolojia," alisema.

"Uongozi unatakiwa kuangalia upya hasa hapa katika motisha ya wachezaji nafikiri kama fedha zinakuwepo na mipango mizuri tunatakiwa kuweka viwango vizuri vya posho katika mechi hizi za CAF ili wachezaji wajitume zaidi tofauti na inavyofanyika sasa naona kama posho za mechi za ndani ni kubwa kuliko zile za mechi za CAF."

Lwandamina alisema mfumo huo tayari hata kwao Zambia ulishaigwa na klabu nyingi kubwa ambapo sasa wameanza kupata matunda hayo kwa kufika mbali katika mashindano hayo makubwa

Aliongeza akisema hatua hiyo itaweza kuipunguzia gharama klabu yao kwa kupata fedha nyingi zinatolewa na CAF katika kufikia hatua mbalimbali ambazo ni nyingi kulingana na aina ya kikosi walicchonacho

"Umeona Zanaco walifanya vizuri katika mashindano yaliyopita wakatutoa lakini wachezaji wao walijituma kutokana na fedha wanazojua watapata endapo watatoa sare au kushinda hiyo ndiyo siri kubwa," alisema.

"Tukijipanga vyema hata klabu itapunguza matumizi ya fedha ukiangalia sasa CAF wamerahisisha safari ya kufika hatua ya klabu kupata fedha za CAF kwa kucheza mechi mbili tu na kutinga makundi. Hakuna kinachoshindikana Yanga tujipange tu," alisema Mzambia huyo aliyeiongoza Yanga katika mechi 53 za mashindano yote tangu ajiunge nayo mwaka mmoja uliopita.