Lukaku atoboa siri ya Mourinho

Muktasari:

Man United tangu 2013 imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England

London, England. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho anajiandaa kupitisha fagio la chuma mwishoni mwa msimu huu na kuna mastaa wasiopungua sita watafunguliwa mlango wa kutokea waende wakatafute timu kwingineko.

Taarifa hizo zinathibitishwa na mshambuliaju namba moja wa timu hiyo, Romelu Lukaku baada ya kufichua kwamba Man United itafanya usajili mkubwa kunasa mastaa wa maana wakati msimu huu utakapofika mwisho.

Lukaku alisema Man United itamwaga fedha ndefu kuhakikisha inasajili mastaa wenye uwezo watakaokuja kuipa nguvu timu hiyo ya kushindana na wababe wengine ndani ya England na Ulaya.

Wachezaji ambao wameshaanza kutajwa kwamba, huenda wakawa miongoni mwa watakaotua  kwenye kikosi hicho cha Old Trafford ni Ivan Perisic, Blaise Matuidi na Marcos Alonso, huku kukiwa na orodha nyingine ndefu inadaiwa kwamba watanaswa na kocha Jose Mourinho kuja kuongeza makali kikosini hapo.

Lukaku, ambaye amefunga mabao 25 msimu huu, anaamini katika usajili huo mpya utakaofanywa utakuja kuiboresha Man United licha ya klabu hiyo imeshatupia Pauni 300 milioni kwenye usajili kwa kipindi kisichozidi miaka miwili.

"Sisi ni Manchester United, tunapaswa kuboresha kiwango chetu bora kila mwaka na nafahamu wazi kwamba, wachezaji wengi waliobora watakuja kwenye dirisha lijalo. Huo ni uhakika," alisema Lukaku.

Man United haina mechi yoyote kwa sasa hadi Machi 31 itakaposhuka uwanjani kucheza na Swansea City kwenye Ligi Kuu England.