Luiza Mbutu awalilia mashabiki

Muktasari:

Mateso wanayoyapata mashabiki wao ni kwenda katika ukumbi huo uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakijua Twanga wapo.

MUIMBAJI mahiri na Kiongozi wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, Luiza Mbutu amesema, mashabiki wao wanateseka kwa sababu hawajui  Ukumbi wa Mango Garden umevunjwa na sasa mambo yapo Vision Plus Lounge.

Mbutu amesema, mateso wanayoyapata mashabiki wao ni kwenda katika ukumbi huo uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakijua Twanga wapo kama ilivyokuwa  wanapiga kila Jumamosi.

“Kiukweli ni tatizo, mashabiki wetu wa Twanga Pepeta walishazoea kila Jumamosi tupo Mango, lakini sasa ukumbi umevunjwa na wengi hawajui,”alisema Mbutu.

“Naomba mashabiki wetu waelewe siku ya Jumamosi Twanga imehamia Ukumbi wa Vision Plus Lounge  (Zamani Miti Mirefu) badala ya Mango Garden ndiko kwenye burudani zote.”

Mbutu alifafanua pia, kwa nini baadhi ya watu walikuwa wanauita ukumbi wa Mango kiwanja cha nyumbani na kusema, sababu ni kwamba, toka uzinduzi wa albamu yao ya kwanza ya Kisa cha Mpemba hadi ya tatu ya Fainali Uzeeni, walizindulia hapo.

“Ni kweli watu wengi wanasema ukumbi wa Mango Garden ni ukumbi wa nyumbani wa Twanga Pepeta,kutokana na albamu zote tatu tulizindulia pale, na sisi tushazoea hivyo”alisema Luiza Mbutu.