Liverpool yamkabidhi Keita mikoba ya Gerrard

Muktasari:

Gerrard ameiongoza Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa 2005

Liverpool, England. Kiungo chipukizi wa Guinea, Naby Laye Keita amekubali kuvaa jezi ya nahodha wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard.

Tangu Gerrard aondoke Liverpool wachezaji wamekuwa wakikwepa kuivaa jezi namba 8, lakini Keita aliyesajiliwa hivi karibuni ameridhia na kuahidi kufanya makubwa kama ilivyokuwa kwa nahodha huyo aliyefanikiwa sana enzi zake.

Mchezaji huyo mwenye miaka 23 aliyesajiliwa kwa Pauni 53 milioni, kutoka RB Leipzig ya Ligi Kuu Ujerumani aliyoitumikia kwa miaka miwili na kufunga mabao 14 katika mechi 58 alizocheza.

 “Kwangu ni heshima sana kukabidhiwa jezi 8 najua inathamani kubwa sana hapa Anfield, ikizingatiwa kuwa mtu wa mwisho kuivaa alikua Steven Gerrard,” alisema Keita.

Alisema atahakikisha anaifanyia Liverpool mambo makubwa kuliko hata alivyofanya akiwa RB Leipzig na moja ya malengo yake ni kutwaa mataji.

Keita amefichua kuwa kutua kwake Liverpool kumekamilisha ndoto ya muda mrefu kwani tangu utoto wake alikua akiishabikia Liverpool sawa na baba yake Sekou, ambaye hadi leo anayo jezi iliyosainiwa na Steven Gerrard.

Kiungo huyo amemshukuru sana Kocha wa Jugen Klopp kwa kumuamini na kumsajili jambo litakalokamilisha ndoto zake.