Liverpool yaichapa Spurs yakaa kileleni

Muktasari:

Hii ni mara ya kwanza kwa Spurs tangu msimu 2015-16 kufunga mechi mbili za mwanza wa msimu

London, England. Liverpool imeendeleza rekodi yake ya ushindi baada ya kuichapa Tottenham Spurs kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Wembley.

Liverpool ikiwa ugenini ilipata bao la kuongoza dakika ya 39, kupitia Georginio Wijnaldum kabla ya Roberto Firmino kuongeza la pili dakika 54, huku bao la kufutia machozi la Spurs likifungwa dakika 90 na Erik Lamela.

 Ushindi huo wa Liverpool ni watano mfululizo msimu huu, huku wakilipiza kisasi cha kufungwa na Spurs kwenye uwanja huo msimu uliopita.

Katika mchezo huo Liverpool ilianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la mapema lililofungwa na Firmino, lakini mwamuzi alikataa akidai mfungaji alikuwa ameotea.

Liverpool inayosaka ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu England tangu ilipofanya hivyo mwaka 1990, ilitawala mchezo huo, lakini washambuliaji wake Mohamed Salah na Sadio Mane walishindwa kutumia vizuri nafasi zao walizopata.