Liverpool ikitoka hapa ubingwa wao

Muktasari:

  • Liverpool inakabiliwa na mechi ngumu sana kwenye Ligi Kuu England baada ya kukamilika kwa mapumziko ya mechi za kimataifa, ambapo itawakabili wababe wengine wa Big Six, Spurs.

LIVERPOOL, ENGLAND. Mshambuliaji XHERDAN Shaqiri amesema anaisubiri kwa hamu kabisa hiyo ratiba ngumu inayoikabili Liverpool kwani hapo hapo ndipo atakapoanza kuwasha moto na kwa kuanzia, atawanyoosha Tottenham Hotspur kesho Jumamosi.

Liverpool inakabiliwa na mechi ngumu sana kwenye Ligi Kuu England baada ya kukamilika kwa mapumziko ya mechi za kimataifa, ambapo itawakabili wababe wengine wa Big Six, Spurs.

Wakinolewa na Mjerumani, Jurgen Klopp, Liverpool imeanza msimu huu vyema kabisa ikishinda mechi zake zote nne za kwanza kwenye Ligi Kuu England na hivyo kushika usukani wa ligi hiyo.

Lakini sasa Spurs ndio inayotajwa itakuwa timu ngumu ya kwanza kwa Liverpool kukabiliana nayo kwenye ligi hiyo msimu huu.

Na Shaqiri akisisitiza yupo vizuri kwa mechi hiyo baada ya kusema: "Naisubiria hii mechi. Wiki zijazo tutakuwa na mechi nyingi sana nzuri na ngumu. Lakini, sisi tutaendelea kucheza kwa ubora wetu na tutaamini tutashinda mechi hizo."

Liverpool itacheza mechi saba ndani ya siku 23, ikianzia kesho Jumamosi itakapoikabili Spurs, kisha itacheza mechi mbili dhidi ya Chelsea na kwenye Ligi ya Mabingwa UIaya inakabiliwa na vigogo Paris Saint-Germain na Napoli.