Liuzio wala hana presha

STRAIKA Juma Liuzio ‘Ndanda’ amesema hana presha yoyote baada ya viongozi wa Simba kumzuia kuondoka klabuni hapo na badala yake ameweka mikakati ya kuhakikisha anaipigania namba yake kwa wachezaji wenzake.

Liuzio aliomba kujiunga kwa mkopo katika klabu mojawapo kati ya Lipuli, Kagera Sugar au Njombe Mji zilizokuwa zinamhitaji kabla ya mabosi wa Msimbazi kumzuia wakitekeleza agizo la kocha, Joseph Omog.

Omog amezuia mchezaji yeyote kuondoka kwa nia ya kutaka kuwa na kikosi kipana kuelekea kwenye michuano mitatu wanayokabiliana nayo; Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika Kombe la Shirikisho, Simba imepangwa kuanza na klabu ya Gendarmerie Tnale ya Djibout katika mechi za raundi ya awali na kama itafuzu itakwaama na ama El Masry ya Misri au Green Buffaloes ya Zambia baadaye katika raundi ya kwanza.

“Ni kweli nilipanga nijiunge na timu nyingine kwa uhamisho wa mkopo ili nipate nafasi ya kucheza mara kwa mara, lakini uongozi umenizuia kwa sababu kocha amependekeza mchezaji yeyote asiondoke kipindi hiki, hivyo nabaki,” alisema.

Kuhusu usajili wa Jonas Sakuwaha kutoka Zambia na ushindani uliopo kikosini mbele ya nyota kama Emmanuel Okwi, John Bocco, Laudit Mavugo na Nicholas Gyan, Liuzio alisema hahofii chochote kwani anauamini uwezo alionao.

“Kikubwa ambacho natakiwa kukifanya kwa sasa ni kujituma na kufanya vizuri zaidi ili nipate nafasi ya kucheza, ila sihofii kabisa ushindani, japo nilipenda kwenda kwingine kujaribu changamoto mpya, napenda kucheza,” aliongeza kusema.

Mbali ya Liuzio, wengine walioomba kuondoka kwa mkopo ni Jamal Mwambeleko na winga Jamal Mnyate ambao nao wamechoshwa na maisha ya benchi kwenye timu hiyo. Ni Mnyate pekee aliyeruhusiwa kutua Lipuli.